KUFIKIA SAATISA ALASILI KURA ZA KUTOKUWA NA IMANI NA PINDA ZILIFIKIA 66

UKUSANYAJI saini za wabunge kwa ajili ya kuwasilisha azimio la kutokuwa na imani na Waziri Mkuu umechangamkiwa lakini kuna mgawanyiko baina ya wabunge wa CCM kwa kuwa baadhi yao wanapinga azimio hilo. 
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe akisaini karatasi inayokusanya saini za wabunge za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha kwa Spika mjini Dodoma. Kulia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto.
 
Hadi jana saa 9 alasiri, wabunge watano wa CCM ndiyo walikuwa wamesaini akiwemo Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, aliyesaini akikanusha kutumwa na mtu kwa kusema hana haja na uwaziri, kama ambavyo baadhi ya wabunge walivyowatuhumu kuwa wanaoshinikiza azimio hilo wanataka uwaziri.


Wanaoponda hoja hiyo wanasema haina mashiko, kwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hahusiki na uteuzi wa mawaziri.


Mbunge aliyezungumza hadharani na waandishi akipinga, ni wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) ambaye amemtetea Pinda kwamba ni mtendaji mzuri na hajavunja maadili yoyote kiasi cha kuruhusu hoja ya kumwondoa kuwa na mashiko.


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) ndiye aliyeongoza kazi hiyo jana na hadi saa 9, zilishakusanywa saini 66 za wabunge kutoka vyama vyote isipokuwa United Democratic Party (UDP) ambacho mbunge wake ni John Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti.


Akiongozana na Filikunjombe, Zitto aliwaambia waandishi wa habari kwamba hadi muda huo, idadi ya wabunge wa CCM waliosaini ni watano, CUF 12 na wengine ni waTLP, NCCR-Mageuzi na Chadema.


Zitto ambaye alionekana akizungusha karatasi ya kusaini kabla ya kumkabidhi pia Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), awazungushie wabunge, alisema hoja hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa kesho kutwa, ni ya wabunge wote huku akisisitiza kwamba si ya upinzani kama inavyoaminika kwa kuwa ilianzia kwa wabunge wa CCM.


“Hii hoja si ya kambi ya upinzani, si hoja ya Zitto, wabunge wa CCM ndio wengi waliolalamika,” alisema Zitto na kusema taarifa zilizopo ni kwamba CUF makao makuu kimewaelekeza wabunge wake wote wasaini.


Hata hivyo, Zitto alitetea udandiaji wa hoja za chama kingine, iwapo zina maslahi kwa wananchi na Taifa. “Katika siasa za kibunge, anayesema hoja imedandiwa, amefilisika…mimi sijafanya hili kama Mbunge wa Chadema. Kuna ubaya gani kama CCM au Chadema ina hoja nzuri mtu kuidandia?” Alihoji.


Zitto ambaye ndiye aliwasilisha juzi bungeni wazo la kuunda azimio hilo, alisisitiza kwamba wabunge wanampenda Pinda isipokuwa mawaziri wake ndio wamemweka rehani iwapo hadi keshokutwa watakuwa hawajachukua hatua za kujiuzulu.


“Tunampenda na kumheshimu sana Waziri Mkuu, lakini pia tunaiheshimu nchi yetu,” alisema na kuongeza kwamba kumpigia kura hiyo, kutaweka historia ndani ya nchi kwani tangu uhuru, hatua kama hiyo haijapata kuchukuliwa. Alipoulizwa kuwa iwapo hoja yao haitapitishwa ni hatua gani watachukua, Zitto alisema Bunge litaingia kwenye historia kwa kuonesha meno.


Taarifa ambazo zimekuwa zikisambazwa, ni kwamba lipo kundi linawatumia baadhi ya wabunge kushinikiza hoja hiyo ipite. “Kuna Mbunge anasambaza uvumi, kwamba watu wamewatuma walete hayo…tusipowawajibishe, wananchi watatudhihaki, tunalinda heshima ya Bunge,” alisema Zitto.


Kwa upande wake, Filikunjombe ambaye alisema baadhi ya wabunge akiwamo yeye, waliitwa jana kushawishiwa kuondokana na kusudio hilo, lakini akawaambia waandishi wa habari kwamba hana mpango wowote wa kutaka kuwa waziri na ikitokea jina lake limewekwa kwenye orodha, ataomba liondolewe.


Msimamo wa wabunge waliosaini ni kwamba lengo la azimio hilo ni kutoka kwenye Bunge la ulalamikaji kwenda Bunge la utendaji ama kwa Waziri Mkuu kuwapisha au kuwawajibisha mawaziri wasiofaa kutokana na ama kuhusika katika ubadhirifu au kushindwa kuudhibiti.