MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amewaasa wananchi kutowauzia ardhi zenye migogoro wawekezaji hasa wazawa.
Kauli hiyo alitoa siku ya Pasaka 8.4.2012 alipokuwa akifungua Hoteli ya kisasa ya Lunch Time Royal Inn iliyopo eneo la Mpemba Tunduma kati ya wilaya ya Mbozi na Momba mkoani Mbeya.
Alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuwauzia baadhi ya wawekezaji maeneo yenye migogoro hali ambayo inawakatisha tamaa wawekezaji wengi hasa wazawa kuwekeza katika mikoa waliyozaliwa jambo ambalo linadidimiza uchumi wa nchi.
‘’Nimefurahi sana kusikio na kuona uwekezaji mkubwa wa aina hii uliofanywa na wazawa na ninatoa rai kuwa waambieni watu wengine wa mkoa wa Mbeya waje wawekeze mkoani kwao kwasababu ni salama na wale wote wenye tabia ya kuwauzia wawekezaji kama hawa maeneo yenye migogoro waache mara moja’’ alisema Kandoro.
Aliongeza kuwa kutokana na uwekezaji wa hoteli hiyo ni dhahili sasa kuwa mkoa wa Mbeya utapata wageni wengi kwasababu hoteli hiyo ina kumbi kubwa tatu ukiwemo wa kutosheleza watu 120,000 na zingine ndogo za kutosheleza watu 200 kila mmoja kwa wakati mmoja huku kukiwa na vyumba vya kulala vya kutosha.
‘’Kutokana na hali hii, naamini hata mikutano ya SADC itafanyika mkoani Mbeya na zaidi mkoa wa Mbeya una vivutio vingi vya utalii na hasa kiwanja cha ndege cha kimataifa kitatuwezesha kukuza uchumi na uwekezaji wa hoteli hii unadhihilisha ni jinsi gani Serikali inaweka mazingira rafiki kati yake na wananchi’’ alisema Kandoro.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hoteli hiyo Frank Mwakatwila alisema ujenzi wa Hoteli hiyo aliuanza miaka miwili iliyopita kwa kukopa fedha kutoka katika benki ya Kenya yenye tawi Jijini Dar es Salaam ijulikanayo kwa jina la NIC na kuamua kuwekeza nyumbani kama kurudisha fadhila na kwamba Hoteli yake itachangia asilimia 30 ya ujenzi unaotarajiwa kujengwa karibu na Hoteli hiyo.
Meneja wa Hotel Hiyo Mathias Mwaipasi alisema kuwa Hotel hiyo mpaka sasa imetoa ajira kwa vijana watanzania hasa vijana wapatao 50 na inatarajia kuajiri jumla ya wafanyakazi 200 kwa ajili ya kupunguza wimbo la ajira nchini