Rais Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo ya aliyekuwa mwigizaji mahiri wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba nyumbani kwake Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
WAKATI utata ukigubika chanzo cha kifo chake, utata mwingine wa wapi atazikwa nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, umeibuka kati ya wazazi wake wawili na wasanii wa tasnia ya filamu.
Hadi sasa, Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia msanii wa kike wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, kutokana na kifo cha Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia juzi.
Polisi katika Mkoa wa Kinondoni, wamesema wanaendelea na uchunguzi wa kifo cha nyota huyo kilichoitikisa Tanzania na kwa taarifa za awali, wanasema chumbani kwake ambako inaaminika ndiko umauti ulimkuta, walikuta panga, pombe ya Whisky ikiwa robo glasi pamoja na soda aina ya Sprite.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema vitu hivyo vilikutwa chumbani kwa Kanumba eneo la Vatican Sinza na kwamba wanaendelea kumhoji Lulu (18), mkazi wa Tabata Relini kuhusu tukio hilo, ambaye alikuwa chumbani pamoja na nyota huyo.
Kenyela alisema Kanumba alifariki juzi saa sita usiku nyumbani kwake ambapo kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Seth Bosco (24), ambaye ni msanii wa kikundi cha The Great Film Production, kaka yake alihitilafiana na Lulu, chanzo kikiwa ni simu.
Alisema Kanumba, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, aliingia chumbani kwake kujiandaa ili watoke, lakini baadaye kidogo aliambiwa na yeye aingie chumbani kwake kwani kuna mgeni anakuja na atakapokuwa tayari atamuita.
Alisema baadaye ndipo mdogo huyo wa marehemu alisikia kelele, kaka yake akimtuhumu Lulu kwa nini anawapigia simu mabwana zake wengine na ndipo ghafla aliitwa na msichana huyo na kuambiwa kwamba akamwangalie kaka yake amezidiwa.
Kenyela alimkariri mdogo huyo akieleza kwamba alipofika chumbani alimkuta Kanumba amelala sakafuni huku akitokwa na povu mdomoni na haongei, ambapo baada ya mawasiliano na daktari wake, alipofika aligundua kwamba alishafariki dunia.
Wakati utata ukigubika chanzo cha kifo hicho, utata mwingine umeibuka kuhusu wapi atazikwa nyota huyo aliyezaliwa Januari 8, 1984 katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, wazazi Flora Mtegoa na baba Charles Kanumba, mfanyakazi wa hospitali hiyo ya Shinyanga.
Wakati Kamati ya Maziko ikieleza kuwa inasubiri uamuzi wa mama yake mzazi ambaye alikuwa akitarajiwa kufika Dar es Salaam wakati wowote jana kutoka Bukoba mkoani Kagera, inapigia debe azikwe katika Makaburi ya Kinondoni katika jiji lililompatia umaarufu mkubwa maishani.
Lakini inadaiwa kwamba mama yake anataka akazikwe Bukoba wakati baba yake jana imekaririwa na taarifa za habari za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), anataka mwanawe huyo akazikwe Mwanza, ambako ndiko kwenye makazi ya babu yake Steven ambaye ndiye
aliyerithi jina la Kanumba.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete amewataka wasanii wa tasnia ya filamu kuendeleza harakati za kuitangaza Tanzania kupitia tasnia hiyo alizozianzisha marehemu Kanumba.
Kikwete alitoa mwito huo kwa wasanii wa filamu jana wakati akizungumza na wasanii mahiri wa Bongo Movie, Vincent Kigosi maarufu zaidi kama Ray na Jackob Stephen nyumbani kwa marehemu Kanumba wakati alipokwenda kutoa rambirambi zake.
Rais Kikwete alisema Kanumba alikuwa ameanza kuwakilisha nchi katika anga za kimataifa katika tasnia ya filamu huku akitumia lugha ya Kiswahili.
Alisema Kanumba ni mfano wa kuigwa kwa vijana, kwa kuwa ametumia muda wake na kipaji chake kuwakilisha nchi katika Bara la Afrika na hivyo kuliletea heshima taifa.
“Ah ninachoweza kusema kuwa ndio hivyo Mungu ameamua kumchukua na sisi wote hatuwezi kuwa na ubishi katika hilo, lakini mimi ninamkumbuka kuwa alikuwa na hali ya kuthubutu na kuhakikisha kuwa analifanikisha lile alilolianzisha,” alisema Rais Kikwete.
“Nakumbuka aliandaa chakula cha mchana kwa kushirikiana na wasanii wenzake pale Dodoma, ambapo nilihudhuria na kuna mengi ambayo niliyafahamu katika tasnia hii kupitia mazungumzo kama hayo,” alisema.
Gazeti hili pia lilimsikia Kikwete akiwasihi akina Ray na JB ambao pia ni viongozi wa kamati za maziko, kuhakikisha kuwa wanakubaliana na kile ambacho wazazi wa Kanumba watataka mahala ambapo mtoto wao azikwe.