RC MBEYA AOMBWA KUINGILIA KATI MGOGORO

 

 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro (Kushoto) akikabidhiwa Mwenge wa uhuru na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stellah Manyanya (kulia), baada ya kumaliza mbio zake mkoani Rukwa.



Wananchi wa kijiji cha Ndembela, Kata ya Makandana Wilayani Rungwe wamemwomba Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kuingilia kati mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kijiji hicho na shule ya sekondari Ndembela inayoendeshwa na Kanisa la Waandiventista Wasabato(SDA) iliyopo kijijini hapo,uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 sasa.


Katika malalamiko yao waliyoyatoa juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa, wananchi hao wamedai kuwa Kanisa hilo la Wasabato limewapora ardhi na majengo ya shule ya Sekondari Ndembera kinyume na matakwa yao, hivyo wamemwomba kandoro kuwasaidia kuirejesha mikononi mwao.


Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kueleza wamesema kuwa katika miaka ya 1980 wakati shule hiyo ikiwa inatoa elimu ya msingi pekee, kulionekana kuwepo na mahitaji ya shule za sekondari na ndipo wakaamua kuibadilisha kuwa shule ya sekondari.


Aidha,baada ya uamuzi huo kupitishwa, Kanisa la Wasabato liliomba kuiendesha shule hiyo kwa ufanisi na Serikali kupitia Kamati ya Maendeleo ya Elimu ya Wilaya ya Rungwe (Rudet) iliikabidhi shule hiyo kwa uongozi wa kanisa hilo.


Wamesema kuwa katika makabidhiano hayo, walikubaliana kuwa kanisa hilo litaiendesha shule hiyo chini ya Halamshauri ambapo ilitakiwa kila mwaka kusomesha wanafunzi wawili bure kutoka vijiji vinavyoizunguka shule hiyo.


Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia madai ya wananchi hao, Solomon Mwakafyaga amesema kuwa baada ya miaka michache kanisa la SDA lilivunja makubaliano hayo na likaanza kufanya utaratibu wa kumiliki shule na majengo ya shule hiyo kinyemela bila wananchi kujua.


Ameyataja baadhi ya mambo yaliyobadilishwa kuwa ni pamoja na vibao vilivyokuwa vimeandikwa awali ‘Shule ya Wananchi’ na kuandikwa ‘Shule ya Waandiventista Wasabato’ ikionyesha kuwa kanisa ndilo wamiliki wa shule, pia kusitisha kusomesha wanafunzi wa kijiji hicho na kuzuia wananchi kupata taarifa za shule kinyume na makubaliano ya awali.


Hivyo wamefikisha madai yao kwa Mkuu wa Wilaya na uongozi wa Halmashauri ambao uliiandikia shule hiyo barua pamoja na kufungua kesi ya madai katika mahakama Kuu kitego cha  ardhi Jijini Dar es Salaam.


Mwafyaga amesema tangu mwaka 1996 wananchi wamekuwa wakitakiwa kusubiri kwa maelezo kuwa kesi ipo mahakamani, lakini wanashangaa kila mwaka shule inaendelea kusajili wanafunzi wa kidato cha kwanza na kidato cha sita, huku wananchi wakiwa hawajui hata tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.


Akijibu hoja hizo toka kwa wananchi, Kandoro amesema kuwa tatizo lao amelichukua na kuomba muda ili alifanyie kazi hivyo kuwataka wananchi hao kuwa na subira na kutousumbua uongozi wa shule hiyo wakati akiendelea kushughulikia tatizo lao.