WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameiba ng’ombe 22 katika kitongoji cha Gezaulole kijiji cha Gwata tarafa ya Mikese mkoani hapa walipokuwa wamepelekwa sehemu ya malisho.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani hapa Adolphina Chialo alisema kuwa ng’ombe hao waliibiwa machi 18 mwaka huu majira ya saa 10 jioni huko katika kijiji hicho.
Alisema ng’ombe hao wenye rangi tofauti walikuwa majike 13 na madume 9 na wanathamani ya sh 14.1 milioni pia ni mali ya Bonifasi Ney (44) mkazi wa Gwata.
Kamanda huyo alisema kuwa paka sasa hakuna mtu anayehusishwa na tukio hilo na wala aliekamatwa na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na wizi huo.
WAKATI HUO HUO mtu mmoja Mbaraka Paza (38) mkazi wa area six manispaa ya Morogoro anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia.
Kamanda Chialo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa machi 20 mwaka huu majira ya saa 6 usiku huko katika nyumba ya kulala wageni iliyokuwa eneo la msamvu.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na noti mbili za shilingi 10,000 kila moja zenye namba BT 1254319 NA BT 1254311 ambazo alikuwa katika harakati za kulipia chumba alichokitumia katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamanni leo lakini pia aliwaasa wafanyabiashara kuwa makini katika sehemu zao za kazi ili kuweza kuwakabili wenye noti hizo na kuweza kuwapeleka katika vyombo vya sheria.