MKUU wa Mkoa wa Arusha awaonya wakurugenzi wenye zarau

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amesema Mkurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Jiji atakayedharau na kushindwa kujibu hoja za ukaguzi wa hesabu atakuwa amejiondoa katika wadhifa wake.

Mulongo aliyasema hayo wakati akihitimisha ziara ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyokagua fedha na miradi katika halmashauri za Monduli na Jiji la Arusha.


Alisema iwapo Mkurugenzi atashindwa kujibu hoja hususani zinazojirudia kwa vipindi tofauti vya ukaguzi atakuwa hafai kuwa mtumishi wa umma kwani anarejesha nyuma juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.


“Haiwezekani Mkurugenzi na wakuu wake wa idara kila wanapokaguliwa hoja ni zile zile na hazijibiwi kwa usahihi…ni wazi kuwa wewe utakuwa hutufai tena, nimeweka makubaliano na wakurugenzi katika hili hatutalaumiana,” alisema.


Alisema matatizo makubwa na yenye kuibua hoja wakati wa ukaguzi ni kukosekana kwa viambatanisho vya taarifa mbalimbali zikiwamo za fedha na utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali za Afya, Kilimo, Elimu na Miundombinu.


Mulongo alionya pia tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kudharau maagizo ya wakaguzi wa hesabu kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambao pamoja na kutoa ushauri na maelekezo mara kwa mara hakuna mabadiliko.


Mjumbe wa Kamati ya LAAC na Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma, Omary Badwel alitaka kila mkuu wa idara katika halmashauri kutekeleza wajibu wake bila kusukumwa na viongozi wengine.