MFANYA BIASHARA wa madini aitwaye Benson Mwakilembe(52)mkazi wa Tazara Mbalizi,leo amefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Mji mdogo wa Mbalizi,kujibu shitaka la kutishia kuua kwa maneno.
Imedaiwa mahakamani hapo mbele ya hakimu mfawidhi , Sofia Fungameza kwamba Mwakilembe alimtishia Chacha Mwita ambaye ni askari wa Jeshi la wananchi Tanzania kuwa atamuua ndani ya siku tano.
Mwita alidai mbele ya hakimu kuwa, alitolewa vitisho hivyo baada ya kuhoji kuhusu kuhamishwa kwa nguzo ya umeme aliyodai kuwa ilihamishwa na Mwakilembe kinyume na taratbu za shirika la umeme nchini (TANESCO).
Kwa upande wa shahidi wa mlalamikaji Mpoki Gwakisa (34) mkazi wa Mbalizi aliieleza mahakama kwamba alifuatwa dukani kwake na mshitakiwa ambaye alimwagiza kwa Mwita kuwa akamweleze kwamba atasambaratisha kijiwe chake na anampa wiki moja ya kuishi.
Ushahidi huo ulionekana kupingana na maelezo yaliyotolewa na mlalamikaji ambaye alidai kuwa Mwakilembe aliahidi kumuua katika kipindi cha siku tano kinyume na maelezo ya shahidi namba moja aliyesema alimsikia Mwakilembe akitamka kwamba atamsambaratisha katika kipindi cha siku saba.
Naye shahidi wa pili ,Cosmas Maluli (50) mkazi wa Tazara Mbalizi alisema kuwa alipigiwa simu na mtoto wake akidai kwamba Mwakilembe amemtukana na kumtishia kumuua,na mnamo machi 9,mwaka huu akiwa mkoani Iringa alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa majirani zake kwamba Mwakilembe aliahidi kumnyoosha.
Mwakilembe alipopewa nafasi ya kuuliza maswali alisema ushahidi uliotolewa na shahidi wa pili haukuwa na ukweli na kudai kwamba maelezo ya shahidi huyo yalikuwa ya kuambiwa wala si ya ana kwa ana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 5 mwaka huu ambapo mshitakiwa ataitolea utetezi mahakamani hapo kuhusu mashitaka yanayomkabiri.