Polisi inawachunguza viongozi sita wa kidini mjini Garissa wakishukiwa kuwashajiisha vijana wa Kenya kujiunga na al-Shabaab, Mkuu wa Polisi wa Jimbo la Kaskazini Mashariki Leo Nyongesa ameiambia Sabahi.
Uchunguzi ulianza Januari na unaendelea, alisema Nyongesa.
“Tumewaita maimamu na wahubiri sita na tupo kwenye mchakato wa kuwahoji wengine,“ alisema. “Tunataka kujua ikiwa wanasaidia katika utoaji mafunzo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa umma zinazoonesha hivyo".
Serikali inasema al-Shabaab imekuwa ikiwafunza vijana kutoka eneo hilo kupigana nchini Somalia kwa miaka kadhaa.
Mwaka 2006, Kamishna wa zamani wa Polisi wa Jimbo la Kaskazini Mashariki, Kiritu Wamae, alisema serikali ilikuwa na majina ya zaidi ya vijana 400 walioorodheshwa katika makundi ya wanamgambo wa kigeni. “Tuna majina ya vijana wa Kikenya ambao wamekuwa wakipata mafunzo ya kupigana nchini Somalia. Familia zimekuwa zikiomboleza kisirisiri,” alisema katika sherehe za Siku ya Kenyatta mjini Garissa.
Aliongezea kuwa serikali ilikuwa na ripoti kuwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo walikuwa wanahusika na uandikishaji huo.
Musa Hussein Abdi, mkazi wa Wajir, alifunguliwa mashitaka hapo mwaka 2007 kwa kumiliki vifaa vinavyotumika kutengeneza mabomu na kuachiwa miaka miwili baadaye kwa kukosekana ushahidi. Mnamo Juni 2011, aliuawa katika mapigano ya risasi na vikosi vya Somalia akiwa na mkuu wa al-Qaeda kwa Afrika Mashariki, Fazul Abdullah Mohammed, ambaye alituhumiwa kupanga mashambulizi ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya ya mwaka 1998.
Vile ile, mkazi mwengine wa Wajir, Said Ali Ibrahim, aliuawa na vikosi vya Somalia mjini Dobley, Somalia, mwezi mmoja kabla.
Sheikh Juma Ngao, mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Waislamu la Kenya, alisema alitoboa siri ya kuwepo kwa uandikishaji wa al-Shabaab katika misikiti ya Kenya kuanzia mwaka 2005.
“Uandikishaji ulifanyika katika baadhi ya misikiti nchini kote, lakini kwa sasa, kwa sababu ya kampeni iliyoanzisha na serikali dhidi ya kikundi cha kigaidi, imesimama,” aliliambia gazeti la Kenya la The Standard mnamo Septemba.
“Lakini inawezekana ikawa unaendelea katika nyumba za watu binafsi," alitahadhaisha. “Baadhi ya maimamu walikuwa wakiwarubuni vijana na wazazi kuwa uandikishaji huo ulikusudiwa kwa vita vitakatifu ilhali wanaua tu watu wasio na hatia.”
“Somalia hakuna jihadi,” alisema, na kuushabihisha uandikishaji wa vijana na biashara haramu ya binadamu kwa migongano ya kimbari, kimakabila, siasa au faida binafsi.
Sheikh Hassan Amey, mwenyekiti wa tawi la Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya, alikubali kuwa kuna wapiganaji wa Kigeni nchini Kenya, lakini alikataa madai kuwa viongozi wa kidini wanajihusisha na uandikishaji kwa ajili ya al-Shabaab.
Viongozi wa kidini na wakazi wamekuwa wakisumbuliwa kwa kisingizio cha kupambana na al-Shabaab,” aliiambia Sabahi.
KWA HABARI ZAIDI (Bofya hapa)