MNYUKANO mkali wa viongozi wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) mkoa wa Mbeya umeendelea na kufikia hatua ya kujipambanua kuwa chama hicho hakina demokrasia tena ambapo viongozi wanapanga uongozi bila kuwahirikisha wanachama wala viongozi wa kata.
Hali hiyo imebainika baada ya uchunguzi wa Gazeti hili kubaini undani wa mnyukano huo ambapo katika wilaya ya Mbeya mjini viongozi wa wilaya wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho John Mwambigija (Mzee wa wa upako) tayari wameshitakiwa ngazi ya mkoa.
Kushitakiwa kwa viongoz hao kumetokana na kuvuruga chama hicho na kupanga uongozi wa kata kwa kile kilichoelezwa kuwa lengo ni kujimilikisha utawala ili katika uchaguzi wa wilaya viongozi hao wachaguliwe tena na ‘’watumwa’’ wao wanaowaweka katika uongozi wa kata za wilaya hiyo.
Viongozi na wanachama wa baadhi ya kata za wilaya hiyo baada ya kubaini mbinu hiyo na uharibifu huo wa kukiuka katiba ya chama hicho na taratibu za uchaguzi wa kata mbalimbali, wameandika barua za malalamiko kwenda ofisi ya mkoa wakieleza jinsi chama hicho kinavyohujumiwa na baadhi ya viongozi wa wilaya.
Baadhi ya barua ambazo Gazeti hili nakala zake imezipata zimetoka katika kata za Iyela, Ruanda na Iganzo zimeutaka uongozi wa mkoa kutengua uchaguzi ambao umefanyika kwa madai kuwa uchaguzi huo haukufuata taratibu bali viongozi wa wilaya walifanya kwa maslahi yao binafsi na kutishia kupoteza wanachama.
Katika barua iliyopokelewa na ofisi ya Chadema mkoa wa Mbeya Februari 22, mwaka huu kutoka kata ya Iyela iliyosainiwa na Esia Edward katibu kata wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekitiwa wa mtaa wa Pambogo imeweka pingamizi la uchaguzi uliofanyika katika kata hiyo Februari 5, mwaka huu.
Barua hiyo imesema kuwa tarehe hiyo viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya walifika katika kata hiyo na kufanya uchaguzi wa papo kwa papo wakati tarehe ya uchaguzi ambayo hata wanachama walitangaziwa na kuchukua fomu za kuwania nafasi za uongozi ilikuwa ni Februari 15, mwaka huu.
‘’Fomu zilizojazwa na wagombea kwa kufuata taratibu hazikutumika na mpaka sasa anazo katibu, badala yake fomu zilihazwa hapohapo ukumbini na wakati wa uchaguzi huo batili, Mwenyekiti wa wilaya aliwaambia wajumbe kuwa viongozi wa kata walimzuia Mbunge kuja Iyela,nahitaji athibitishe’’ imeeleza barua hiyo.
Barua hiyo imeendelea kusema kuwa ‘’Nikiwa kama Katibu kata, nataka kufahamu fomu zilizolipiwa kwa utaratibu kwa utaratibu uliopangwa na mkutano Mkuu wa kata nizipeleke wapi? Pia wale wanachama tuliovuna toka 2011-2012 na wamejaza fomu niwajibu nini ili wabaki kuwa wanachadema’’ imeeleza barua hiyo na mengine mengi.
Mbali na kata ya Iyela pia uongozi wa kata ya Iganzo umeiomba ofisi ya mkoa kutengua matokeo ya uchaguzi uliofanyika Februari 10, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wa Wilaya na kaimu Katibu wa chama hicho wilaya.
Katiba barua hiyo kipengele cha © (i) imeeleza kuwa Mwenyekitiwa wilaya kugawa vyeo ‘’ Mtu ambaye hakugombea nafasi hiyo-Diwani wa Iganzo alipata kura 3 katika nafasi ya Uenyekiti wa Baraza la wazee Kata ya Iganzo ambapo mgombea mwenzake alipata kura 24’’
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti mnachelewa kutekeleza tunayowaandikia hamkitendei haki chama chetu haki, kwani uongozi wa Chadema Mbeya Mjini upo kujijengea himaya ya wateule na wateule na wengineo na siyo kujenga chama’’ imeeleza barua hiyo.
Sanjari na hayo imeendelea kusema kuwa viongozi na wanachama hao wanatambua fika kuwa Mwenyekiti wa chama hicho wilaya anaamua kufanya hivyo ili kuandaa mazingira ya kuchaguliwa katika nafasi ua Uenyekiti wilaya hivi karibuni kupitia kwa viongozi wa kata anaowaweka sasa pasipo kufuata taratibu.
Barua hiyo iliyosainiwa na S.D.Kabuka imeendelea kusema kuwa ‘’Nahisi laghai zake zinazima ushauri wetu na uwezo wa mkoa kuyaratibu yaliyo sahihi kwa chama, ona hata Katibu Mkuu Taifa alivyoingizwa mkenge’’ imesema bila kufafanua mkenge alioingizwa Dr. Wilbroad Slaa na Mwenyekiti huyo na uhusiano wao kwa ujumla.
Kwa upande wa wanachama wa kata ya Ruanda na viongozi wa chama hicho katika kata hiyo nao wamepeleka barua katika ofisi ya mkoa huo wakipinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Februari 14, mwaka huu badala ya Februari 27, huku wakiwashutumu Mwenyekiti wa wilaya, Katibu wa wilaya, katibu Mwenezi wilaya na kaimu katibu wazee.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba CDM/MBY/M/2012/5 na kusainiwa na katibu kata Ruanda Binadamu L. Mwatujobe, imesema kuwa uongozi uliochaguliwa chini ya viongozi hao wa wilaya hautambuliki na wameiomba ofisi ya mkoa kuutengua na kupaleka kamati ndogo ya kusimamia uchaguzi maana hawana imani tena na uongozi wa wilaya uliopo hivi sasa.
Sanjari na migogoro hiyo ambayo ipo ndani ya chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini, chama hicho wilaya ya Mbeya Vijijini nachi kinakabiliwa na minyukano mikali ambapo baadhi ya viongozi wameendelea kupimana nguvu za maamuzi huku Mwenyekiti wa wilaya hiyo Elia Kabolile akishutumiwa kutumia vibaya fedha za ruzuku za chama hicho hivyo kutishiwa kung’olewa.
na Kalulunga