WATU WATATU WAFARIKI MORO


  • MWANAUME AANGUKIWA NA GOGO

WATU watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Morogoro likiwemo la mwanaume mmoja kuangukiwa na gogo la mti wakati akichana mbao porini katika eneo la Tununguo Tarafa ya Ngerengere wilayani Morogoro.


Kamanda wa polisi mkoani Morogoro Adolphina Chialo amesema jana ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea februali 19 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni katika eneo hilo.


Kamanda huyo amesema kuwa mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina moja la Mustapha anayekadiriwa kuwa umri kati ya miaka (30-40) alifariki dunia papo hapo baada ya kuangukiwa na gogo la mti wakati akichana mbao katika pori hilo.


KATIKA TUKIO LA PILI kijana mmoja Wilson Chawia (34) mkazi wa kitange wilayani Gairo amefariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kuacha njia na kugonga nyumba.


Kamanda huyo amesema kuwa tukio hilo limetokea februali 18 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana katika maeneo ya Iyogwe wilayani humo.


Amesema kuwa kijana huyo wakati akiwendesha pikipiki hiyo yenye nambaza usajili T 281 AVG aina ya SUNLG akiwa amempakia abiria aliyefahamika kwa jina la Samuel Chawia (16) mkazi wa Kitange akitokea kijiji cha Chakwale kuelekea Gairo aligonga nyumba hiyo na kusababisha kifo chake papo hapo na abiria aliyempakiza kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya misheni Berega.


Hata hivyo kamanda huyo amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa pikipiki hiyo.

WAKATI HUO HUO mkazi mmoja wa kijiji cha Mbokwa wilayani Morogoro Dini Utomola (33) amefariki dunia baada ya kunywa sumu ya panya.


Kamanda Chialo amesema kuwa tukio hilo lilitokea februali 19 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi katika kijiji hicho kilichopo kata ya mikese wilayani humo.


Kamanda huyo amesema kuwa mtu huyo alifariki dunia akiwa katika hospitali ya Rufaa mkoani hapa akipatiwa matibabu ambapo chanzo cha kunywa sumu hiyo bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi.