WAPATIWA MAFUNZO YA UTUNZAJI WA FEDHA



IMEELEZWA kuwa mafunzo ya kuweka nidhamu ya matumzi na utunzaji wa  fedha yanayotolewa na Shirika Mama la CNFA kutoka nchini Marekani kupitia mradi wa farmer to farmer yatawasaidia  kwa kiasi kikubwa mawakala kuwanusuru kufilisiwa kutokana na kushindwa kurejesha mikopo wanayokopa katika taasisi mbalimbali za fedha.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Chama cha Mawakala wa Pembejeo,Wilaya ya Njombe,Waziri Kindamba wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mafunzo hayo yaliyoanza (Febr,16)mjini hapa.

Kindamba alisema kuwa mawakala wengi wamekumbwa na dhahama ya kufilisiwa mitaji na mali zao  kutoka katika maeneo waliyokuwa wakikopa kutokana na kutojuwa utunzaji wa fedha pamoja na nidhamu katika matumizi ya fedha za biashara  na hivyo kujikuta wakitumia hata fedha  ambazo siyo zao.

"Mawakala walio wengi walishindwa kurejesha fedha za mkopo  kutokana na kushindw akutofautisha  faida na mtaji,unakuta wakala amekopa mzigo wa sh.mil.100 alafu akiuza pembejeo anaziona zile fedha kama zake,"alisema

Aliongeza," anachukuwa Sh.Mil.40 ananunua gari ama nyumba kumbe pale faida yake ni Sh.Mil.5 zile Mil.95 ni mtaji ambao siyo wake ni mkopo kwa hiyo anajikuta anaingia katika matatizo anafilisiwa na mwisho makampuni yanakataa kutukopesha."

Alitolea mfano mblolea aina ya DAP inayouzwa Sh.72 ambapo baada ya kuuza wakala anapata faida ya sh.1,000 lakini kutokana na kukosa elimu ya nidhamu ya matumizi na utunzaji wa kumbukumbu za fedha anajikuta anaiona fedha yote kama yake na kuitumia.

Mhasibu wa Chama hicho,Sergius Mlowe amelishukuru Shirika la CNFA kwa kuwapatia mafunzo hayo  ambayo yatamfanya wakala  aweze kuandika taarifa yake ya fedha  na mtiririko wa fedha  wenye mpangilio mzuri  kwani mali bila daftari upotea bila habari.

Mwenyekiti wa NAC,Andrea Sanga alisema elimu watakayoipata itawasaidia kuwajengea ujasiri wa kuweza kuingia katika taasisi na makampuni ya fedha kukopa kwania watakuwa wamepata uelewa mpana wa nidhamu katika fedha.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amewaomba wakulima kuwaunga mkono pindi wanapofikishiwa pembejeo vijijini  badala ya kuwavunja nguvu  hasa pale mawakala wanapoongeza Sh.1,000 katika pembejeo ikiwa ni gharama za usafiri.