WAKAZI wa mkoa wa Rukwa wametakiwa kutumia majiko yanayotumia kuni na mkaa kidogo ili kupunguza uharibifu wa mazingira katika mkoa huo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Mohamed Gharib Bilal, alitoa rai hiyo jana katika mkutano wa Hadhara katika uwanja wa kumbu kumbu ya Nelson Mandela mjini Sumbawanga

Alisema hivi sasa mkoa wa Rukwa umeanza kupoteza misitu mingi kutokana na kushamiri kwa vitengo vya uharibifu wa mazingira katika maeneo mengi ya mkoa huo vinavyochangiwa na shughuli mbali mbali za binadamu

Alisema kuchoma moto kiholela kunachangia sana kuua mbegu za miti na misitu mingi kuendelea kuteketea kwani miti iliyopo nayo inaendelea kuteketezwa na wachoma mkaa pamoja na matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia.

“hivi sasa ukipita katika maeneo karibu yote vijijini hasa vijiji vya wilaya ya Sumbawanga kumebaki upara licha ya kuwa maeneo hayo yalikuwa na misitu minene tena ya kutisha” alisema Dr Bilali

Alisema umefika wakati wananchi wa Rukwa waanze kubadili tabia na kuona suala la uharibifu wa mazingira kuwa ni sawa na janga la mkoa mzima na lianze kushughulikiwa kwa mikakati maalumu itakayosimamiwa vema na kupunguza uharibifu uliopo sasa.

Alisema kuwa moto kichaa ni moto ambao unachomwa pasipo misingi ya kiutaalamu kwani hata wanaosafisha mashamba wanatumia kuchoma moto na kuuacha unaendelea kuangamiza misitu mingine 

Katika mkoa wa Rukwa kumekuwa na utamaduni wa kuchoma moto hasa nyakati za kiangazi kwa lengo la kuwinda, kuchimba panya, kusafisha mashamba baada ya kuvuna mazao pamoja na kutenga maeneo ya kuchungia mifugo yao.

Maeneo yaliyoathirika na uharibifu wa mazingira kwa kiwango kikubwa ni pamoja na wilaya ya Nkasi, Sumbawanga vijijini , wilaya ya kalambo na kata za Inyonga, Kasokola, Mpanda mjini, Magamba, Nsimbo, 
Uruila na Mtapenda katika wilaya ya Mpanda.