JESHI la polisi mkoani Rukwa linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili kwa sababu za kishirikina katika kijiji cha Usevya wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa alisema jana kuwa waliokamatwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili wanaendelea kuhojiwa zaidi kabla ya kuwafikisha mahakamani huku jeshi hilo likiendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine waliokimbia baada ya mauaji hayo.

Alisema mnamo Februari 21, 2012 majira ya saa tatu usiku watu wasiojulikana waliwavamia Consolata Nsokolo (64) na Oliva Pesambili (74) katika kijiji cha Usevya na kuanza kuwashambulia kwa mapanga, mawe na marungu kwa madai kuwa walikuwa wameroga mvua isinyeshe kwa muda wa mwezi mzima kijijini hapo.

Alisema watu hao waliweza kuwavamia na kuwaua wazee hao kisha wakatokomea kusikojulikana ambapo katika vurugu hizo watu wawili Eliasi Ngomarufu (58) na Modesti Nsokolo (71) walijeruhiwa walipoajaribu kuwaokoa ndugu zao wasiuawe 

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa alisema kuwa tukio hilo lilihusisha imani za kishirikina kwani wauaji walikuwa wakiwatuhumu marehemu hao kuwa ni wachawi wameroga mvua isinyeshe katika eneo lote la kijiji hicho kwani mvua ilikuwa haijanyesha kwa zaidi ya mwezi mmoja .

Alisema wananchi waache kuendekeza imani za kishirikina na kuchukua hatua ambazo kimsingi na ukikaji wa sheria na kueleza kuwa hivi sasa kuna mabadiliko ya hali ya hewa mabadailiko ambayo yanapelekea mambo mengi kutokea kama vile radi, upepo mkali, mafuriko na hata ukame wa muda mrefu.

Alisema licha ya kuwa mvua inayodaiwa kukosekana kwa muda mrefu ilinyesha siku moja baada ya mauaji na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao kwani mvua hiyo iliambatana na mawe yaliyochana chana mazao si kweli kuwa waliouwawa walikuwa wamezuia mvua isinyeshe.