Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi ya kitabu cha mtafiti bingwa duniani wa Masokwe, Jane Goodall, aliyefika Ikulu ndogo ya Wlaya ya Mpanda mkoa wa Katavi jana kwa ajili ya mazungumzo. Jane amekaa nchini kwa miaka 50 akifanya utafiti katika mapori ya Gombe na Mahale yaliyopo mkoa wa Kigoma na Katavi.
Habari na Mwandishi wetu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Mohamed Gharib Bilal anatarajia kuwasili Jijini Mbeya leo kwa ziara ya siku tatu ambapo jumla ya miradi minane itafunguliwa.
Akiongea na waandishi wa habari ofisi kwake mkuu wa mkoa wa Mbeya Abasi Kandoro amesema Dokta Bilal anatarajiwa kuwasili Jijini hapa mapema siku ya Ijumaa akitokea Mkoani Rukwa ambapo atatembelea Wilaya za Mbozi, Mbarali, Rungwe na Wilaya ya Mbeya.
Akiwa mkoani hapa Dokta Bilali atafungua soko la wafanyabiashara Tunduma, kutembelea shule ya sekondari Vwawa ambapo atazindua rasmi matumizi ya Teknolojia ya maabara rafiki na kuzindua ofisi ya CCM eneo la Mlowo.
Aidha ataweka jiwe la msingi katika jengo la Saccos ya UWAMU iliyopo eneo la Uyole, kufungua kituo cha mafunzo ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Simambwe Mbeya Vijijini, pamoja na kuweka jiwe la msingi katika hosteli ya Jiji iliyopo eneo la Sokomatola.
Akiwa wilayani Mbarali atakagua miradi miwili ya ujenzi wa bwawa la umwagiliaji pamoja na ujenzi wa soko la mpunga katika eneo la Igurusi, wilayani Rungwe atafungua ofisi ya Muungano wa wakulima wadogo wadogo wa Chai wilayani humo, kufungua mradi wa umwagiliaji na kutembelea shamba darasa katika vijiji vya Kisegese Kasyabone.