KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida ziara ya Mheshimiwa Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Anne Makinda imeingia dosari baada ya mkutano alioufanya hivi karibun kuingia dosari baada ya wananchi kuzomea na kudhira kuendelea kumsikiliza.
Hali hiyo imetokea Februari,21 mwaka huu katika mfulululizo wa ziara za Mheshimiwa spika Makinda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Njombe kusini kupita kuzungumza na wapiga kura wake katika mitaa mbalimbali ya mjini Njombe.
Kama ilivyo ada Makinda amekuwa akiendesha mikutano yake kwa mfumo wa wananchi kuuliza maswali ambapo katika mitaa aliyopita alikumbana na swali la kuhusu kuzorota kwa mfumo wa ugawaji wa vocha za pembejeo za ruzuku.
Dosari iliingia katika mkutano wake uliofanyika Mtaa wa national Housing,Kata ya Mji Mwema ambapo baada ya kuulizwa swali lilihusu pembejeo, na kuhamishwa kwa madereva eneo la stendi ya malori, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe,Edwin Mwanzinga aliomba alijibu.
“Zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo za ruzuku limeingia dosari baada ya Mawakala wa Pembejeo kutuingiza mjini kwa kutuuzia bei kubwa…hapa mjini kuna wapumbafu…mjini shule usipende ulivyolelewa wewe na wengine walelewe hivyo hivyo,mimi nawatolea ufafanuzi wananchi wa mtaa wa National Housing kama haunielewi niite pembeni nikueleweshe,”alisikika Mwenyekiti huyo.
Kufuatia kauli hiyo wananchi walizomea na kuondoka kwa hasira na kumuacha Mbunge wao Mh.Makinda na baadhi ya viongozi alioambatana nao wakipigwa na butwaa huku wananchi wakilalamikia udanganyifu anaosema Mwenyekiti huyo huku wao wakielewa sababu kubwa ya kuchelewa kwa pembejeo ni serikali.
Awali Spika wa Bunge,alitolea ufafanuzi swali lililohoji kuhusu sababu inayofanya bunge linaloongozwa na Makinda kuonekana kutokuwa na nidhamu ambapo alijibu limejaa vijana wadogo wavulana na wasichana.
“Asilimia 70 ya wabunge katika Bunge la tisa wamepoteza viti na hivyo asilimia 70 ya waliokuja ni wapya na wengi wao ni vijana wadogo ni wasichana na wavulana tena kwa wasichana nimelazimika kutenga na ukumbi kwa ajili ya kunyonyeshea ndiyo wanaanzza kuzaa…nimefungisha ndoa kadhaa,”alifafanua.
Aliongeza:”kwa hiyo vijana hawa walipokuja kwa mara ya kwanza bungeni hawakujuwa taratibu,hawanakuwa na uzoefu walidhani kupiga kelele kama walivyozoea wakati wa kampeni katika majukwa ya kisiasa na bungeni vivyo hivyo ndiyo maana mkasikia tufunge milango tupigane.”
Mheshimiwa makinda alifafanua kuwa Bunge katika umoja wake katika mataifa yote duniani kuna utaratibu,sheria na kanuni zake katika kusema,kuuliza swali,kupiga makofi na kutamka maneno na kadhalika hivyo vijana wameanza kuzoea na kuendelea kuelimishwa na hali ya utulivu inarejea.
Aidha Makinda katika ziara yake mtaa wa Joshoni aliahidi kutoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa wa huo.