Annan ateuliwa mjumbe maalumu kwa mzozo wa Syria

Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa Syria, kabla ya kuanza kwa mkutano wa "Marafiki" wa Syria mjini Tunis utakaojadili mgogoro wa nchi hiyo.

 Bwana Annan ameteuliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu. Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu wamesema jukumu la Bwana Annan litakuwa kukomesha mauaji na kukiukwa haki za binadamu na kuhimiza juhudi za kuleta suluhisho la amani. Uteuzi wa Annan ulifanyika kabla ya mazungumzo ya mjini London ambako, kwa mujibu wa taarifa, Marekani, Ulaya na nchi za Kiarabu zilitayarisha onyo kali kwa Rais Assad, la kumtaka akubali kusimamisha mashambulio mara moja au atawekewa vikwazo madhubuti. Majeshi ya Rais Assad yamekuwa yanaushambulia mji wa kati wa Syria, Homs, kwa muda wa karibu wiki tatu sasa. Hata hivyo Urusi na China zimesisitiza kwamba zinapinga ujiingizaji wowote kutoka nje katika mambo ya Syria. Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 70 na mashirika ya kimataifa wanatarajiwa kushiriki katika mkutano wa mjini Tunis.