MCHUNGAJI AKUTWA AKIWANGA NYUMBANI KWA MTU
MCHUNGAJI wa Kanisa la .. lililopo Iyunga mkoani hapa, Geophrey Joram hivi karibuni alikutwa akiwanga nyumbani kwa Amanyisye Fungo mkazi wa Inyala jijini Mbeya .
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwao kijana aliye jitambulisha kwa jina la Baraka Amanyisye (17) alisema kuwa ,mnamo Februari 8 mwaka huu majira ya saa moja asubuhi alimkuta mchungaji Joram mlangoni kwao akinyunyiza kimiminika ambavyo kinachosadikika kuwa ni dawa za kienyeji.
Alisema kwamba, baada ya mchungaji huyo kukutwa mlangoni hapo na kijana huyo aliondoka na kuelekea Kanisani kwake ambako ni jirani na nyumba aliyokutwa akinyunyiza maji yanayoaminika yalikuwa ni dawa ya kuidhuru familia ya nyumba hiyo.
Baraka alisema kuwa kabla ya kitendo cha mchungaji huyo hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya familia yao na mchungaji huyo na baada ya kumkuta akifanya kitendo hicho kilipelekea kujenga hofu na kumfuata mama yake ili kumpasha habari hizo.
Naye mama wa kijana huyo alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kwamba ,baada ya kupokea taarifa hizo aliamua kwenda kutoa taarifa kwenye ofisi za serikali ya mtaa wa Inyala ambako waliamua kwenda katika eneo la tukio kisha kumfuata mchungaji Joram ili kutoa maelezo kuhusiana na tukio hilo.
Mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Tuvi Kyando(48)alisema kuwa baada ya viongozi wa mtaa kufika katika eneo la tukio waliamua kumwita mchungaji huyo lakini hakuweza kuitikia wito huo badala yake aliamua kukimbia na kwaacha watu wakimshangaa huku wengine wakiamini kwamba alikuwa na nia mbaya katika tukio hilo.
Alisema kwamba,viongozi wa mtaa walifanya jitihada ya kumsimamisha lakini hawakufanikiwa badala yake aliwajibu watakutana kituoni na alijibu hivyo huku akitimua mbio na kutokomea kusikojulikana hadi MWISAE Blogu inaingia mitamboni mchungaji huyo taarifa zake zinasema hajawahi kufika kanisani hapo wala hajulikani mahali alipo.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliohojiwa na mwandishi wetu walikiri kuwepo kwa tukio hilo lakini wakidai kuwa wao sio wasemaji wa kanisa hivyo hawakuwa tayari kuelezea kwa kina tukio hilo ingawa pia walithibitisha kuwa mchungaji wao kakimbilia kusikojulikana baada ya kutishiwa kuuawa.
Habari zaidi juu ya mkasa wa mchungaji Joram,zinasema kwamba siku mbili baada ya tukio hilo waumini wa kanisa hilo walikwenda kanisani hapo kung’oa mabati ya jengo la kanisa hilo lakini walizuiliwa na serikali ya mtaa ambayo ilimwita askofu wa kanisa hilo ili kusikia mawazo yake juu ya uamuzi wa waumini wake.
MWISAE Blogu ilibahatika kuingia kwenye kikao kilichokaa majira ya saa 7 mchana kwenye ofisi ya afisa mtendaji wa kijiji cha Inyala ambacho kiliketi na askofu wa kanisa hilo ,Emanuel Tumwidike na uongozi wa kijiji hicho pamoja na familia ya Amanyisye Fungo ambaye ni mwenye mji alikokutwa mchungaji akiwanga.
Kikao hicho kilimtaka askofu Tumwidike atoe tamko rasmi kuhusu kitendo alichokifanya mchungaji wake Joram ,askofu huyo alikiri kuitwa mara mbili kijijini hapo kusuruhisha migogoro ya mchungaji wake na wakazi wa eneo hilo ambao walikuwa wakilalamikia huduma za mchungaji huyo ikiwa ni pamoja na kudai kupigishwa kelele usiku wa manane.
Askofu huyo alisema kuwa ,mchungaji huyo hakuwa na nia mbaya bali alikuwa akipaka mafuta ya upatanisho na familia ya Fungo ambayo ilikuwa ikisigana na mchungaji huyo na chanzo kikiwa ni mipaka ya ardhi ya mji wa Fungo na eneo la Kanisa,lakini baadae alikiri kuwa mchungaji alifanya kosa kwa sababu alifanya kitendo hicho bila ya taarifa kwa mlengwa.
Tamko rasmi la askofu Tumwidike alisema kuwa kwa kuwa waumini wameamua kung’oa mabati yao na iwe hivyo,uongozi wa mtaa ulitoa kibali cha kung’oa mabati hayo ambapo mji utaendelea kushikiliwa na muumini aliye likodisha kanisa hilo.
Habari zaidi za uchunguzi katika eneo la Inyala zinasema kwamba jambo lolote baya likijitokeza katika familia ya Fungo linaweza kuzua mapigano kati mchungaji huyo kwani hadi sasa hawana imani na mchungaji kwa madai kuwa mchungaji huyo amekuwa akiliendesha kanisa katika misingi ya kishirikina.
Jitihada za kumpata mchungaji huyo ili kuelezea tuhuma hizo zilishindikana kwani tangu alipokimbia katika eneo la tukio bado haijafahamika alikoelekea ingawa kuna habari zisizo aminika kuwa mchungaji huyo amefichwa na kimada wake aliyetajwa kwa jina moja la Elizabeth ambaye pia inasemekana kuwa ni muumini wake.