Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evans Balama, amesema kuwa serikali imeshtushwa na tukio la mvua kubwa za mawe zilizonyesha katika kijiji cha Nsambya Songwe na kuharibu hekari 248 za chakula na kuziacha familia 68 zikiwa hazina kitu.
Balama amesema alipokuwa akipokea msaada wa mifuko 100 ya saruji iliyotolewa na kampuni ya Tunakopesha Limited tawi la Mbeya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa mtaa wa Ikuti, kata ya Iyunga waliokumbwa na mafuriko makubwa Desemba mwaka jana.
Akipokea msaada huo toka kwa meneja wa tawi hilo, Job Mwakyoma, kwa ajili ya waathirika wawaliobomokewa nyumba 22, vyoo 30 na nyumba nyingine 40 kuharibika, Balama amesema msaada huo utawawezesha baadhi ya wananchi kuweza kujenga upya makazi yao.
Alieleza madhara ya mvua hiyo iliyonyesha kwa muda wa saa 18 kwa wakazi wa kijiji cha Nsambya kuwa ziliharibu hekari 248 za mazao zikiwa ni 122 za mahindi, 96 za maharage, 17 nukta 5 za kahawa na 10 nukta 5 za migomba.