MUFA KUFANYA UCHAGUZI
CHAMA cha soka mjini Mbeya (MUFA) kinatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu februari 25, 2012 mjini Mbeya, baada ya viongozi waliokuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mine kumaliza muda wao.
Taarifa ya kufanyika kwa uchaguzi huo unaosubiriwa kwa kwa hamu kubwa na wadau pamoja na mashabiki wa soka wa mjini Mbeya, ilitolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa uchaguzi Sambwee Shitambala alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.
Shitambala ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema kuwa miaka ya nyuma uchaguzi wa Mufa, ulikuwa unafanyika kiholela bila ya kufuata taratibu za TFF, lakini hali hiyo kwa sasa imefanyiwa marekebisho.
Alisema katika miaka ya nyuma wagombea walikuwa wanapitishwa pasipo kuonyesha vyeti vya elimu zao, kitu ambacho kimechangia sana kurudisha nyuma maendeleo ya soka mjini Mbeya.
Shitambala alisema kwa utaratibu wa sasa mwanasheria ndiye atakaye kuwa mwenyekiti wa uchaguzi, na kwamba anaiamini kamati yake kwa vile ina watu waelewa.
Mwanasheria huyo aliwataja watu wanaounda kamati hiyo ya uchaguzi kuwa ni Inspekta Ntabahanyi wa jeshi la Magereza ambaye ni katibu, na yeye mwenyewe kama Mwenyekiti.
Aliwataja wajumbe wakamati hiyo kuwa ni M.P. Mwambe ambaye ni Meneja wa Ukumbi wa mikutano wa Mkapa, na Mkurugenzi wa redio ya Sweet Fm ya jijini Mbeya, Emmanuel Mbuza na Mjumbe mwingine ambaye hakuweza kulikumbuka jina lake.
“Nataka nifanye kazi pamoja na kamati yangu kwa umakini mkubwa, ili safari hii Mbeya iweze kupata watu wakuendeleza michezo”, alisisitiza Shitambala.
Shitambala aliongeza kuwa watasimamia vigezo vyote vya elimu kwa wagombea wote, na kamati pia itaangalia kama mgombea anacheti cha kidato cha nne au lah! Na kwa wale watakao kosa sifa hizo hawata ruhusiwa kugombea.
Alizitaja na fasi zitakazo gombewa kuwa ni ile ya Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, Katibu mkuu, Katibu msaidizi, Mtunza hazina na zile za Mjumbe wa mkutano Mkuu wa Mkoa, Mjumbe mwakilishi wa vilabu, wajumbe watatu wa kamati tendaji ambao jumbla yao ni kumi.
Usaili ulifanyika Jumamosi ya Februari 4 na uchaguzi umepangwa kufanyika Februari 25 kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, na waliorejesha fomu, za uchaguzi mpaka sasa wamefikia 17.
Mwisho
MASHINDANO ya ligi ya Rahatele kwa vilabu vya daraja la Tatu na vile vya mchangani vya mjini Mbeya, yalizinduliwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari Mkoani Mbeya Christopher Nyenyembe.
Uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Baa Tugelepo uliopo katika maeneo ya Ghana Jijini hapa, Ulihudhuriwa na viongozi wa vilabu 17 kati ya 20 vitakavyo shiriki mtanange huo pamoja na waandaaji wa mashinda hayo kutoka kampuni ya Misha Communications.
Viongozi wa timu walioshiriki katika uzinduzi huo ni watimu za Uswazi Fc, Aljazeela, Town Star, Terminal Fc, Jangwani Fc, Nakivubo Fc, South Camp, Zaragoza Fc, Vinega Fc, na Nyota Fc.
Wengine ni Majengo Fc, Market Fc, Samaki Fc, Mbaspo Fc, Itiji Fc, Old Forest, Pamoja na Kiongozi wa timu ya Inter-Forest Fc zote za mjini Mbeya.
Akizindua mashindano hayo yatakayo anza kutimua vumbi Februari 15 mwakahuu katika viwanja vya shule za msingi za Mbata na Itiji zote za Mjini hapa, Nyenyembe alisema kuwa siku hizi mpira ni ajira na sifa za wachezaji ni kuibua vipaji vipya.
Alisema mkoa wa Mbeya ni maarufu kwa michezo na hilo halina ubishi, kwani mkoa huu pia umejipatia umaarufu katika michezo ya Ndondi, Kandanda, Riadha pamoja na Muziki wa aina mbalimbali.
Kiongozi huyo wa wana habari Mkoani Mbeya alisema kuwa mashindano yajayo ya Rahatele anaimani kubwa kuwa yatazalisha vipaji vipya kupitia kwa vijana.
Nyenyembea alitoa rai kuwa wachukuliwe vijana wenye uwezo wa kucheza mpira, kwani msingi mzuri katika mashindano yoyote yale yanatokana na maandalizi mazuri.
“Wanamichezo tunatakiwa kuwa kielelezo cha kulinda usalama wetu na kama lengo la mashindano hayo ni kucheza mpira, basi tucheze mpira,” alisema Nyenyembe kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa kama ligi hii ni ya vijana yosso basi wachezaji wakongwe (Vijeba) walio cheza katika ligi kuu wasihusishwe, kwa sababu lengo kuu la mashindano haya ni kuibua vipaji.
Aliitimisha kwa kusema kuwa mashindano haya lazima yaendeshwe kwa nidhamu kama njia mojawapo, ya kuyaboresha na kuongeza msisimuko kwa timu zitakazo shiriki.
Bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kikombe, seti ya Jezi na kitita cha Tsh 200,000/=, wakati wapili atapata pia seti ya Jezi na Tsh 100,000/=, watatu atapata jezi za juu pekee na Tsh 50,000/=, wakati mshindi wa nne atapata mpira na Tsh 20,000/=.
Naye Mdhamini wa mashindano hayo Muddy Lalika alisema kuwa timu yenye nidhamu bora itapata Tsh 20,000?=, mfungaji bora wa ligi hiyo atapata Tsh 20,000/=, wakati kipa bora atajiwekea kibindoni 20,000/= na mwamuzi bora atapata Tsh 20,000/=.
mwisho