Showing posts with label June 30. Show all posts
Showing posts with label June 30. Show all posts
MSIMAMO WA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU KAULI YA JPM KWA WANAFUNZI WALIOJIFUNGUA

MSIMAMO WA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU KAULI YA JPM KWA WANAFUNZI WALIOJIFUNGUA

TAMKO LA PAMOJA LA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU KUWAPA FURSA WASICHANA KURUDI SHULENI BAADA YA KUJIFUNGUA: #ArudiShule
Sisi asasi za kiraia nchini Tanzania tumeungana kwa pamoja kuzungumzia umuhimu wa kuwapa watoto wa kike fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua. Nia yetu ni kuona wasichana wakipata fursa zitakazowawezesha kufikia ndoto zao na kuwa na maisha bora. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 asilimia 51 ya watanzania ni wanawake na wasichana. Chochote kinachowaathiri kundi hili kinaliathiri taifa zima. Kuwaelimisha wasichana na wanawake kunalihakikishia Taifa maendeleo endelevu.
Ni muhimu ifahamike kwamba wasichana wa kitanzania wanakabiliwa na vikwazo vingi katika safari yao ya kupata elimu ikiwemo mazingira duni ya kujifunzia, kutozingatiwa kwa mahitaji maalumu ya watoto wa kike, unyanyasaji wa kijinsia na umbali mrefu kati ya makazi na shule.
Zaidi ya kwamba sisi ni Asasi za Kiraia nchini Tanzania pia ni wazazi, wanajamii na wazalendo, hivyo tunaiomba Serikari yetu itusikilize.
Wananchi wanasemaje?
Kwa mujibu wa utafiti wa Sauti za Wananchi (2016) asilimia 71 ya watanzania wanasema wasichana wapewe fursa ya kurudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Ikumbukwe kwamba elimu katika shule za umma hugharamiwa na kodi za wananchi ambao ndio waliotoa maoni hayo.
Sera zetu, ahadi zetu na viongozi wetu wanasemaje?
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kilichopewa dhamana ya kuliongoza taifa letu inatamka wazi kwamba wasichana waliopata mimba watapewa fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua. Pia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014 inatamka bayana kwamba Serikali itaondoa vikwazo vya elimu kwa watoto wote nchini Tanzania.
Vile vile tunatambua kwamba Serikali ilikua na dhamira ya kuona wasichana hawa wanapata haki ya kuendelea na masomo. Sisi AZAKI tulishirikiana na Serikali katika mchakato wa kutengeneza sera na miongozo itakayowawezesha wasichana hawa kuendelea na masomo katika utaratibu rasmi. Hivyo basi tunaomba nia hii njema iendelee.
Sheria zetu zinasemaje?
Chini ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria nyingine za nchi yetu mtoto anatambulika kama mtu yeyote mwenye chini ya umri wa miaka 18. Sheria hizi zinatoa haki ya watoto wote kupata elimu bila ubaguzi wa aina yeyote ikiwemo ujauzito. Na ikumbukwe Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa misingi ya sheria.
Wasichana wanasemaje?
Si kweli kwamba wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni ni wahalifu wanaostahili adhabu ya kukatishwa ndoto zao. Wengi wao hawana elimu sahihi juu ya haki na wajibu wao na ni wahanga wa matukio ya ubakaji. Sheria zetu zimetamka wazi kwamba kushiriki tendo la ngono na mtoto chini ya miaka 18 ni ubakaji. Tafiti zinaonesha kwamba wasichana watatu kati ya kumi walishiriki tendo la ngono kwa mara ya kwanza bila ridhaa yao. (UNICEF, CDC and MUHAS, 2009) zaidi ya nusu ya wasichana hao walisema wahusika waliotekeleza ubakaji huo ni watu wenye nguvu kuwazidi; ambapo asilimia 32 ni majirani, asilimia 15 ni wenye mamlaka juu yao na asilimia 7 ni ndugu zao.
Tunaomba ifahamike kwamba ujauzito si changamoto pekee inayowakabili wasichana kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kuliko wavulana katika safari yao ya kupata elimu. Kupata ujauzito na kupitia misukosuko ya uzazi katika umri huu ni adhabu tosha, kuwanyima fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua ni kuwaongezea ugumu wa maisha yao wenyewe pamoja na watoto waliowazaa.
Jamii inafaidakaje?
Akina mama walioelimika wana nafasi kubwa ya kujenga jamii endelevu. Takwimu zinaonesha akina mama walioelimika hujifungulia katika vituo vya afya kwa msaada wa watalaam jambo ambalo hupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ukilinganisha na wale wasio na elimu. Vile vile utafiti wa Uwezo (2015) unaonesha kuwa watoto ambao mama zao wana elimu wanafanya vizuri kwenye masomo kuliko wale ambao mama zao hawana elimu.
Kumnyima mtoto wa kike elimu kuna madhara makubwa kwani mwanamke asiyeelimika anakabiliwa na ugumu wa hali na mali katika malezi na makuzi ya mtoto. Pia tufahamu kwamba ni vigumu kwa raia asiyeelimika kushiriki katika shughuli za kuingiza kipato na hivyo kuwa tegemezi kwa jamii na Taifa.
Majirani zetu wanasemaje?
Nchi jirani ikiwemo Kenya wana sera na miongozo inayowawezesha wasichana kurudi shuleni baada ya kujifungua hivyo tunaweza kujifunza kutoka kwao. Visiwani Zanzibar,tangu mwaka 2010 wasichana wanaopata ujauzito wanawezeshwa kurudi shule kwa utaratibu maalum kama mkakati wa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo. Katika nchi zinazotekeleza sera hii hakuna ushahidi wa kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaopata ujauzito kwa sababu ya kusoma pamoja na wasichana waliojifungua.Visiwani Zanzibar kiwango cha wasichana wanaopata mimba za utotoni ni asilimia 8 tu ukilinganisha na asilimia 27 Tanzania Bara (Tanzania Health and Demographic Survey 2015-6).
Sisi tunasemaje?
Tunatambua kwamba, serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati na thabiti kabisa ya kuleta maendeleo katika Taifa letu kwa kutoa fursa sawa za elimu kwa watoto wa Kitanzania pasipo ubaguzi; na isingependa kuona lengo hili halitimii. Tunaomba waliangalie jambo hili upya na kulitafutia ufumbuzi.
Na kwa hitimisho, tunaomba mijadala juu ya suala hili isizuiliwe. Tunaamini watafiti, vyombo vya habari, viongozi wa dini na watanzania kwa ujumla wana maoni yanayohitaji kusikilizwa. Masuala yenye maslahi ya kitaifa yanahitaji mjadala wa kitaifa ili kuleta tija kwa Taifa.
Imepitishwa na:
1. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
2. HakiElimu
3. Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
4. Msichana Initiative
5. Tanzania Education Network / Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET)
6. Twaweza
7. Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA)
8. Child Dignity Forum (CDF)
9. Women Action Towards Economic Development (WATED)
10. East Africa Law Society
11. Engender Health
12. Young Strong Mothers Foundation (YSMF)
13. TAMASHA
14. AGAPE AIDS CONTROL PROGRAMME
15. C-SEMA
16. AFRIYAN
17. YAM – UMATI
18. Centre Against Gender Based Violence
19. Youth for Change – Tanzania
20. Tanzania Peace, Legal Aid and Justice Centre (PLAJC)
21. Caucaus for Children’s Rights (CRC)
22. Hope Riser Organisation
23. New Hope New Winners Foundation (NHWF)
24. Tanzania Media Women’s Association (TAMWA)
25. + Other 50 members of Tanzania Human Rights Defenders’ Coalition (THRDC) working on women and child rights from across the country.
26. Women in Law and Development in Africa (WilDAF)
27. Mkakati Action
28. Restless Development
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sYVlEl
via IFTTT


MWANAMKE ASIMULIA ALIVYOBAKWA KWA ZAMU SIKU YA HARUSI YAKE

MWANAMKE ASIMULIA ALIVYOBAKWA KWA ZAMU SIKU YA HARUSI YAKE

Wakati Terry Gobanga, wakati huo akiitwa Terry Apudo alipotoweka katika harusi yake hakuna mtu aliyedhani kwamba alitekwa nyara, kubakwa na kutuwa kandakando ya barabara akipigania uhai.
Lilikuwa janga la kwanza kati ya mawili kumkabili muhubiri huyo kijana. Lakini ni manusura.
Harusi iliopangwa ilitarajiwa kuwa harusi kubwa.
Nilikuwa muhubiri hivyobasi wanachama wote wa kanisa walitarajiwa kuhudhuria.
Mchumba wangu Harry na mimi tulikuwa na furaha tulikuwa tunafunga ndoa katika Kanisa la All Saints Cathedral mjini Nairobi na nilikuwa nimekodisha rinda zuri sana la harusi. Lakini usiku kabla ya ndoa yetu, niligundua kwamba nina baadhi ya nguo za Harry .
Asingeweza kuja katika harusi bila tai kwa hivyo rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa amekubali kubaki nami usiku wa kuamkia harusi alikubali kumpelekea mapema alfajiri.Terry Gobanga
Niliamka mapema na kumpeleka hadi katika kituo cha kupanda basi.
Nilipokuwa nikirudi nyumbani, nilipita karibu na mtu mmoja ambaye alikuwa ameketi kati boneti ya gari na akanishika kutoka nyuma na kuniingiza katika viti vya nyuma vya gari hilo na kuondoka mahali hapo.
Yote haya yalifanyika kwa sekunde moja. Nilifunguliwa mdomo na kuwekwa kipande cha nguo mdomoni.
Nilikuwa nikirusha mikono na miguu nikitaka kupiga kelele. Nilipofanikiwa kutoa kitambara hicho nilipiga kelele, ni siku yangu ya harusi! hapo ndipo nilipopigwa ngumi .
Mmoja ya wanaume hao wakaniambia nishirikiane nao ama niuwawe. Wanaume hao walinibaka kwa zamu .
Nilihisi nitafariki, lakini bado niliendelea kupigania uhai wangu, hivyo basi mtu mmoja alipotoa kitambara kilichokuwa mdomoni mwangu nilimuuma uume wake.
Alipiga kelele kwa uchungu na mmoja wao akanidunga kisu tumboni.
Baadaye walifungua mlango na kunitupa kando ya barabara huku gari likiendelea kwenda. Nilikuwa mbali na nyumbani, nje ya jiji la Nairobi .
Ilikuwa zaidi ya saa sita baada ya kutekwa. Mtoto mmoja aliniona nikirushwa nje ya gari na akamweleza bibiye.
Watu walikuja mbio. Wakati maafisa wa polisi walipokuja walijaribu kuangalia iwapo bado ninapumua, lakini hawakuona kama nilikuwa bado napumua.
Wakifikiri nimefariki walinitia katika blanketi na kuanza kunipeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti .
Lakini njiani nilikohowa. Polisi mmoja alisema, bado hajafariki, hivyobasi wakabadilisha njia ya kuelekea katika chumba cha kuhifadhi maiti na kunipelekea katika hospitali kuu ya serikali nchini Kenya.
Niliwasili nikiwa na mshangao mkubwa, nikizungumza mambo nisioelewa. Nilikuwa nusu uchi nikivuja damu huku sura yangu ikiwa na majeraha kutokana na kipigo nilichopata.Kanisa la All saints Cathedral Nairobi
Lakini kuna kitu kimoja kilichomshtua mwanamke aliyekuwa akisimamia matibabu, kwa sababu aligundua mimi ni bibi harusi.
”Twendeni kanisani tuone iwapo wanamkosa bibi harusi”, aliambia wauguzi.
Kwa bahati kanisa la kwanza waliloulizia ni All Saints Cathedral jijini nairobi ambapo waliambiwa kwamba kulikuwa na harusi mwendo wa saa nne Asubuhi lakini bibi harusi hakuonekana.
Chanzo: bbcswahili
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sYVK9N
via IFTTT


RAIS MAGUFULI APELEKA KILIO KWA MBUNGE JOSHUA NASSARI

RAIS MAGUFULI APELEKA KILIO KWA MBUNGE JOSHUA NASSARI

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joshua Nassari huenda bado hajaelewa nini kielikumba jimbo hilo baada ya Diwani wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema kuwa anamuunga mkono Rais Dkt Magufuli.
Diwani huyo wa CHADEMA ambaye ni watano kujiuzulu katika jimbo hilo, alisema jana wakati akitangaza uamuzi huo kuwa, ameridhishwa na utendaji kazi wa kiongozi huyo wa nchi na kwamba kazi anayoifanya ni nzuri na inatakiwa kuungwa mkono na watu wote.
Aidha, Kifukwe alisema kuwa, hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa, na kwamba anataka kufanyakazi zake binafsi kwani siku zote amekuwa msema kweli akipigania maendeleo ya wananchi wake.
Muda mfupi baada wa diwani huyo kujiuzulu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kuwa kiongozi huyo na wengine wote wamekuwa wakinunuliwa na CCM katika mkakati wake wa kuidhoofisha CHADEMA, na kwamba wao hawawezi kumzuia kiongozi aliyeamua kununuliwa kwa fedha.
“Nimejiuzulu mwenyewe na sitarajii kujiunga na chama kingine cha siasa bali nataka kufanya kazi zangu mwenyewe. Nimeona kazi anazofanya Rais ni nzuri ambazo hata wapinzani tulitaka kuzifanya,” alisema Kifukwe akikanusha madai ya Lema kuwa amenunuliwa na CCM.
Madiwani wengine wanne waliokuwa wamejiuzulu kabla yake ni, Diwani wa Leguruki, Anderson Sikawa, Diwani wa Mikamba, Emmanuel Mollel, Diwani wa Maroroni, Greyson Isangya na Diwani wa Viti Maalum, Josephine Mshiu wote kutoka jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Aloyce Hhayuma alisema kuwa, madai kwamba madiwani hao wamenunuliwa na CCM si ya kweli bali wamehama na wangine kuachia nyadhifa zao kutokana na kuvutiwa na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Hili ni pigo kubwa kwa CHADEMA mkoa wa Arusha kufuatia madiwani hao kujiuzulu kwani watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanashinda viti hivyo wakati wa chaguzi ndogo.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2ur6Ge2
via IFTTT


KAULI YA WAZIRI MKUU KUHUSU MAENDELEO YA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

KAULI YA WAZIRI MKUU KUHUSU MAENDELEO YA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeadhimia kupambana vilivyo dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa historia nchini.
Pia ametoa wito kwa wazazi wote nchini waendelee kufuatilia nyendo za watoto ili wasijiingize kwenye mtego wa dawa za kulevya na wala wasisubiri vijana wao waanze kutumia.
Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Juni 29, 2017) kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini Dodoma.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa kikamilifu nchini.
Amesema katika kutimiza azma hiyo, ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuanzisha chombo cha kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo imeongeza adhabu kwa wanaoshiriki.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza mapambano ya dawa za kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na kwa kutumia mbinu za kisayansi.
“Tunaponadi uchumi wa viwanda lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza kushiriki kwenye kazi halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka kudhohofisha nguvu kazi ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa viwanda atashughulikiwa bila huruma,” amesema.
Aidha, kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’
Waziri Mkuu amesema kauli mbiu hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.
“Hili ndilo kundi kubwa kwenye jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi wa nchi yetu. Hili ndilo kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu, wanasiasa wa kuongoza Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia Tanzania,” amesema.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema matumizi ya dawa za kulevya yamelisababishia Taifa madhara makubwa ya kiafya na kiuchumi hivyo kila mwananchi ashiriki katika mapambano hayo.
Mapema Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la Kituo cha Kutoa Huduma ya Tiba kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya katika eneo la Itega mkoani Dodoma na kuwashauri wakazi wa mkoa huo kutojihusisha na biashara hiyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama dawa mbalimbali za kulevya katika maonyesho yaliyokwenda sambamba na Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la Kituo cha Kutoa Huduma kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya mjini Dodoma Juni 29, 2017. Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga
Wasanii wa Kikundi cha Mchoyi cha Dodoma wakicheza ngoma ya kabila la Wagogo katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za ulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Gaudensia Simwanza wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke akizungumza katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017
Baadhi ya wananchi na Viongozi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980, DODOMA.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2stE2YE
via IFTTT


CCM NA EDWARD LOWASSA KATIKA MVUTANO MWINGINE

CCM NA EDWARD LOWASSA KATIKA MVUTANO MWINGINE

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepinga vikali kauli iliyotolewa na mwanasiasa mkongwe hapa nchini kuhusu Masheikh wa Uamsho kikisema kuwa kauli hiyo ni ya kidi ni na kichochezi.
Chama hicho kimeitaka serikali kutofumbia macho watu wa hivyo na kwamba endapo watathibitisha kuwa kauli hiyo haikuwa na mrengo mzuri katika jamii, wasisite kumchukulia hatua mhusika mkuu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Humphrey Polepole ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema chama hicho kinalaani kauli iliyotolewa na Lowassa katika futari aliyokuwa amealikwa.
Katika futari hiyo, Lowassa aliwataka waislamu nchini kutokuwa wa baridi wakaishia tu kuongea badala yake watafute lugha nyingine ambayo wakizungumza serikali itaielewa ili viongozi wa dini hiyo wanaoshikiliwa kwa miaka minne sasa waweze kuachiwa.
Kufuatia kauli hiyo ambayo Polisi walisema kuwa ni ya kichochezi, Lowassa aliitwa na tayari kuhojiwa na Polisi siku ya Jumanne na alitakiwa kurudi tena leo. Alipokwenda leo mahojiano hayo yalishindakana kufanyika kwa madai kuwa upelelezi dhidi yake haujakamalika na hivyo kutakiwa kurejea Julai 13.
Katika hatua nyingine, Polepole amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaunga Mkono Kauli ya Rais Magufuli ya kutorudi masomoni kwa wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule kwenye mfumo rasmi wa Elimu.
Polepole amesema kuwa wanafunzi waliopata ujauzito hawataweza kurudi shuleni kwenye mfumo rasmi isipokuwa kwenye Mfumo wa elimu ya watu wazima.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2soCROG
via IFTTT


Chagua Kufanya Mambo Haya, Ili Yakupe Mafanikio Makubwa

Chagua Kufanya Mambo Haya, Ili Yakupe Mafanikio Makubwa

Siku zote maisha ya binadamu yanaongozwa na uchaguzi tunaoufanya kila siku. Uchaguzi huo ndio unatufanya tuwe na maisha haya au yale. Kama uchaguzi unaoufanya ni mbovu kila siku, basi ni wazi na maisha yatakuwa mabovu vilevile. Na kama uchaguzi wako ni mzuri, halikadharika na maisha yako yatakuwa mazuri vivyo hivyo.
Kitu cha kuwa makini nacho hapa, angalia uchaguzi unaoufanya kila siku na kila wakati. Uchaguzi huo ndio unaoamua maisha yako ya kesho yaweje. Kama ni hivyo, ni lazima kwetu kufanya uchaguzi utakaotupa maisha bora. Jaribu kujiuliza, ni uchaguzi wa mambo gani unaotakiwa kuufanya ili kukupa mafanikio makubwa?
1. Chagua kutumia fursa vizuri.
Kwa fursa yoyote inayojitokeza mbele yako, jifunze kuitumia vizuri. Kama ni fursa ya kibiashara au elimu itumie vizuri mpaka uone mafanikio yake. Acha kucheza na fursa yoyote ya kimafanikio inayojitokeza mbele yako. Ikiwa utafanya hivyo elewa ni lazima ipo siku utakuja kujuta kwa uamuzi ulioufanya leo.
Kuna watu ambao wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokuwa makini na fursa zilizojitokeza kwao. Bila shaka umeshawahi kuwaona watu hawa ambao wana majuto na majonzi makubwa kila wakikumbuka ujinga walioufanya. Hili ni tatizo linalosababisha ndoto za wengi kukwama. Ili ufanikiwe, jifunze kutumia kila fursa vizuri.
2. Chagua kuishi na watu chanya.
Siku zote ukiwa mtu wa kuishi na watu hasi basi ni wazi utapata matokeo wanayopata watu hao. Kama ni kulalamika, kulaumu ama kukosa mafanikio, utapata matokeo kama hayohayo. Hakuna kikubwa utakachoweza kukibadilisha. Mara nyingi maisha yetu yanathiriwa sana na wale watu wanaotuzunguka.
Siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye watu wanaokuzunguka pia. Sio rahisi kuishi na watu hasi, halafu ukategemea mafanikio, sahau hilo. Ni lazima watakurudisha nyuma. Watu wenye mafanikio makubwa wanalijua hili. Hata wewe ukitaka kufanikiwa chagua kuishi na watu chanya. Utajifunza mengi huko na utafika mbali kimafanikio.
3. Chagua kufanya kazi kwa bidii.
Kitu kitakachokutoa hapo ulipo na kukufanikisha ni kufanya kazi kwa bidii. Kazi yoyote unayoifanya jitoe kuifanya kwa nguvu zote mpaka uifanikishe. Acha kufanya kazi kwa mkono mlegevu utajikwamisha kwenye kwa mambo mengi kuliko unavyofikiri. Ile hali ya uvivu uliyonayo jitahidi uitoe na kisha endelea kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii.
Watu wenye mafnikio makubwa siku zote wanafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuona mipango na malengo yao yanatimia. Kumbuka hakuna kitu utakachokipoteza ikiwa utajitoa kwa moyo kufanya kazi zako kwa bidii. Zaidi utajiongezea ujuzi, maarifa na uzoefu mkubwa utakaoutumia leo na kesho kwa maisha yako.
4. Chagua kukabiliana na matatizo na kuyashinda.
Tatizo lolote unalokabiliana nalo unao uwezo wa kulishinda. Hakuna tatizo lilokubwa kwako ambalo linaweza likakushinda. Kwa kulijua hilo chukua jukumu la kuchagua kukabiliana na tatizo lako na acha kuruhusu hata kidogo hilo tatizo likakushinda.
Tumia uwezo wako mkubwa wa akili uliopewa, tafakari kisha tafuta njia sahihi za kuweza kukabilana na tatizo lako. Kwa kufanya hivyo utakuwa mshindi na hakuna ambacho kitashindikana kwao. Wanamafanikio wote siku zote huwa ni watu wakukabiliana na matatizo yao na siyo kuyakimbia.
5. Chagua kujifunza.
Ipo haja ya kutafuta mafanikio huku ukiwa unajifunza. Unapojifunza inakusaidia kujua mambo mengi sana ambayo utayatumia katika safari yako ya mafanikio. Huu ni uchaguzi muhimu sana kuufanya ili kujihakikishia nafasi kubwa ya mafanikio katika maisha yako. Jifunze kupitia vitabu, semina au warsha mbalimbali itakusaidia sana.
Hivi ndivyo ambavyo unaweza ukachagua mambo haya na yakawa nguzo na msaada mkubwa wa mafanikio siku zote.
Nikutakie ushindi katika safari yako ya mafanikio na kumbuka tupo pamoja.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2u5YQap
via IFTTT


Kategori

Kategori