Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joshua Nassari huenda bado hajaelewa nini kielikumba jimbo hilo baada ya Diwani wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema kuwa anamuunga mkono Rais Dkt Magufuli.
Diwani huyo wa CHADEMA ambaye ni watano kujiuzulu katika jimbo hilo, alisema jana wakati akitangaza uamuzi huo kuwa, ameridhishwa na utendaji kazi wa kiongozi huyo wa nchi na kwamba kazi anayoifanya ni nzuri na inatakiwa kuungwa mkono na watu wote.
Aidha, Kifukwe alisema kuwa, hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa, na kwamba anataka kufanyakazi zake binafsi kwani siku zote amekuwa msema kweli akipigania maendeleo ya wananchi wake.
Muda mfupi baada wa diwani huyo kujiuzulu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kuwa kiongozi huyo na wengine wote wamekuwa wakinunuliwa na CCM katika mkakati wake wa kuidhoofisha CHADEMA, na kwamba wao hawawezi kumzuia kiongozi aliyeamua kununuliwa kwa fedha.
“Nimejiuzulu mwenyewe na sitarajii kujiunga na chama kingine cha siasa bali nataka kufanya kazi zangu mwenyewe. Nimeona kazi anazofanya Rais ni nzuri ambazo hata wapinzani tulitaka kuzifanya,” alisema Kifukwe akikanusha madai ya Lema kuwa amenunuliwa na CCM.
Madiwani wengine wanne waliokuwa wamejiuzulu kabla yake ni, Diwani wa Leguruki, Anderson Sikawa, Diwani wa Mikamba, Emmanuel Mollel, Diwani wa Maroroni, Greyson Isangya na Diwani wa Viti Maalum, Josephine Mshiu wote kutoka jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Aloyce Hhayuma alisema kuwa, madai kwamba madiwani hao wamenunuliwa na CCM si ya kweli bali wamehama na wangine kuachia nyadhifa zao kutokana na kuvutiwa na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Hili ni pigo kubwa kwa CHADEMA mkoa wa Arusha kufuatia madiwani hao kujiuzulu kwani watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanashinda viti hivyo wakati wa chaguzi ndogo.
from Blogger http://ift.tt/2ur6Ge2
via IFTTT