MSIMAMO WA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU KAULI YA JPM KWA WANAFUNZI WALIOJIFUNGUA

TAMKO LA PAMOJA LA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU KUWAPA FURSA WASICHANA KURUDI SHULENI BAADA YA KUJIFUNGUA: #ArudiShule
Sisi asasi za kiraia nchini Tanzania tumeungana kwa pamoja kuzungumzia umuhimu wa kuwapa watoto wa kike fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua. Nia yetu ni kuona wasichana wakipata fursa zitakazowawezesha kufikia ndoto zao na kuwa na maisha bora. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 asilimia 51 ya watanzania ni wanawake na wasichana. Chochote kinachowaathiri kundi hili kinaliathiri taifa zima. Kuwaelimisha wasichana na wanawake kunalihakikishia Taifa maendeleo endelevu.
Ni muhimu ifahamike kwamba wasichana wa kitanzania wanakabiliwa na vikwazo vingi katika safari yao ya kupata elimu ikiwemo mazingira duni ya kujifunzia, kutozingatiwa kwa mahitaji maalumu ya watoto wa kike, unyanyasaji wa kijinsia na umbali mrefu kati ya makazi na shule.
Zaidi ya kwamba sisi ni Asasi za Kiraia nchini Tanzania pia ni wazazi, wanajamii na wazalendo, hivyo tunaiomba Serikari yetu itusikilize.
Wananchi wanasemaje?
Kwa mujibu wa utafiti wa Sauti za Wananchi (2016) asilimia 71 ya watanzania wanasema wasichana wapewe fursa ya kurudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Ikumbukwe kwamba elimu katika shule za umma hugharamiwa na kodi za wananchi ambao ndio waliotoa maoni hayo.
Sera zetu, ahadi zetu na viongozi wetu wanasemaje?
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kilichopewa dhamana ya kuliongoza taifa letu inatamka wazi kwamba wasichana waliopata mimba watapewa fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua. Pia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014 inatamka bayana kwamba Serikali itaondoa vikwazo vya elimu kwa watoto wote nchini Tanzania.
Vile vile tunatambua kwamba Serikali ilikua na dhamira ya kuona wasichana hawa wanapata haki ya kuendelea na masomo. Sisi AZAKI tulishirikiana na Serikali katika mchakato wa kutengeneza sera na miongozo itakayowawezesha wasichana hawa kuendelea na masomo katika utaratibu rasmi. Hivyo basi tunaomba nia hii njema iendelee.
Sheria zetu zinasemaje?
Chini ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria nyingine za nchi yetu mtoto anatambulika kama mtu yeyote mwenye chini ya umri wa miaka 18. Sheria hizi zinatoa haki ya watoto wote kupata elimu bila ubaguzi wa aina yeyote ikiwemo ujauzito. Na ikumbukwe Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa misingi ya sheria.
Wasichana wanasemaje?
Si kweli kwamba wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni ni wahalifu wanaostahili adhabu ya kukatishwa ndoto zao. Wengi wao hawana elimu sahihi juu ya haki na wajibu wao na ni wahanga wa matukio ya ubakaji. Sheria zetu zimetamka wazi kwamba kushiriki tendo la ngono na mtoto chini ya miaka 18 ni ubakaji. Tafiti zinaonesha kwamba wasichana watatu kati ya kumi walishiriki tendo la ngono kwa mara ya kwanza bila ridhaa yao. (UNICEF, CDC and MUHAS, 2009) zaidi ya nusu ya wasichana hao walisema wahusika waliotekeleza ubakaji huo ni watu wenye nguvu kuwazidi; ambapo asilimia 32 ni majirani, asilimia 15 ni wenye mamlaka juu yao na asilimia 7 ni ndugu zao.
Tunaomba ifahamike kwamba ujauzito si changamoto pekee inayowakabili wasichana kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kuliko wavulana katika safari yao ya kupata elimu. Kupata ujauzito na kupitia misukosuko ya uzazi katika umri huu ni adhabu tosha, kuwanyima fursa ya kurudi shuleni baada ya kujifungua ni kuwaongezea ugumu wa maisha yao wenyewe pamoja na watoto waliowazaa.
Jamii inafaidakaje?
Akina mama walioelimika wana nafasi kubwa ya kujenga jamii endelevu. Takwimu zinaonesha akina mama walioelimika hujifungulia katika vituo vya afya kwa msaada wa watalaam jambo ambalo hupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ukilinganisha na wale wasio na elimu. Vile vile utafiti wa Uwezo (2015) unaonesha kuwa watoto ambao mama zao wana elimu wanafanya vizuri kwenye masomo kuliko wale ambao mama zao hawana elimu.
Kumnyima mtoto wa kike elimu kuna madhara makubwa kwani mwanamke asiyeelimika anakabiliwa na ugumu wa hali na mali katika malezi na makuzi ya mtoto. Pia tufahamu kwamba ni vigumu kwa raia asiyeelimika kushiriki katika shughuli za kuingiza kipato na hivyo kuwa tegemezi kwa jamii na Taifa.
Majirani zetu wanasemaje?
Nchi jirani ikiwemo Kenya wana sera na miongozo inayowawezesha wasichana kurudi shuleni baada ya kujifungua hivyo tunaweza kujifunza kutoka kwao. Visiwani Zanzibar,tangu mwaka 2010 wasichana wanaopata ujauzito wanawezeshwa kurudi shule kwa utaratibu maalum kama mkakati wa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo. Katika nchi zinazotekeleza sera hii hakuna ushahidi wa kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaopata ujauzito kwa sababu ya kusoma pamoja na wasichana waliojifungua.Visiwani Zanzibar kiwango cha wasichana wanaopata mimba za utotoni ni asilimia 8 tu ukilinganisha na asilimia 27 Tanzania Bara (Tanzania Health and Demographic Survey 2015-6).
Sisi tunasemaje?
Tunatambua kwamba, serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati na thabiti kabisa ya kuleta maendeleo katika Taifa letu kwa kutoa fursa sawa za elimu kwa watoto wa Kitanzania pasipo ubaguzi; na isingependa kuona lengo hili halitimii. Tunaomba waliangalie jambo hili upya na kulitafutia ufumbuzi.
Na kwa hitimisho, tunaomba mijadala juu ya suala hili isizuiliwe. Tunaamini watafiti, vyombo vya habari, viongozi wa dini na watanzania kwa ujumla wana maoni yanayohitaji kusikilizwa. Masuala yenye maslahi ya kitaifa yanahitaji mjadala wa kitaifa ili kuleta tija kwa Taifa.
Imepitishwa na:
1. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
2. HakiElimu
3. Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
4. Msichana Initiative
5. Tanzania Education Network / Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET)
6. Twaweza
7. Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA)
8. Child Dignity Forum (CDF)
9. Women Action Towards Economic Development (WATED)
10. East Africa Law Society
11. Engender Health
12. Young Strong Mothers Foundation (YSMF)
13. TAMASHA
14. AGAPE AIDS CONTROL PROGRAMME
15. C-SEMA
16. AFRIYAN
17. YAM – UMATI
18. Centre Against Gender Based Violence
19. Youth for Change – Tanzania
20. Tanzania Peace, Legal Aid and Justice Centre (PLAJC)
21. Caucaus for Children’s Rights (CRC)
22. Hope Riser Organisation
23. New Hope New Winners Foundation (NHWF)
24. Tanzania Media Women’s Association (TAMWA)
25. + Other 50 members of Tanzania Human Rights Defenders’ Coalition (THRDC) working on women and child rights from across the country.
26. Women in Law and Development in Africa (WilDAF)
27. Mkakati Action
28. Restless Development
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sYVlEl
via IFTTT