MAZAO MATANO YANAYOINGIZIA SERIKALI FEDHA ZA KIGENI ZAIDI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kufufua mazao matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni nchini.
Amesema mbali ya korosho, Serikali imeamua kuboresha mazao ya tumbaku, chai, kahawa na pamba.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana na leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maeneo mbalimbali akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora.
Alisema kuanzania sasa serikali imepiga marufuku matumizi ya dola za Marekani kwenye ununuzi wa zao la tumbaku kwa sababu mazao mengine makuu hapa nchini yananunuliwa kwa fedha za Kitanzania.
“Ni kwa nini tumbaku inunuliwe kwa dola za Marekani ilhali mazao mengine yananunuliwa kwa fedha za Tanzania? Korosho, pamba, chai na kahawa wakulima wetu kote huko wanalipwa kwa fedha za Tanzania, kwa nini tumbaku iwe tofauti?” alihoji.
Alisema wenye makampuni wanaweza kukaa kwenye vikao vyao na kupanga bei zao kwa dola za Marekani lakini pindi wanapoingia nchini, watalazimika kufanya malipo kwa kutumia fedha ya Tanzania kwani mfumo malipo kupitia dola za Marekani umekuwa ukiwaibia wakulima kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amewataka watendaji na watumishi wa Halmashauri na wilaya za mkoa wa Tabora wasimamie zao la tumbaku ili kuinua kilimo cha zao hilo na kuwanufaisha wakulima.
“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mnapaswa kulisimamia zao hili na siyo kuwaachia maafisa wa makampuni yanayonunua tumbaku.” 
“Kwa muda mrefu mlizembea na kuwaachia maafisa wa makampuni ya ununuzi ndiyo washughulike na wakulima. Nataka mbadilike, kuweni karibu na wakulima na muwasaidie kulima kisasa na kwa kutumia pembejeo,” alisema.
“Wasaidieni wakulima watoke kwenye mfumo wa kukopa pembejeo, wahimizeni wajiwekee akiba ili msimu ukianza wawe na fedha ya kununua pembejeo. Wakulima wanalaliwa sababu ya mikopo ya pembejeo. Makato yanakuwa mengi kiasi kwamba mkulima ahambulii chochote,” alisema.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kaliua ambako atazungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.

from Blogger http://ift.tt/2w0kws1
via IFTTT