DAR ES SALAAM: Hii inauma sana! Wakati wengi wakitamani kuingia kwenye ndoa ili kuyafurahia maisha hayo, kwa binti Zai Mkiwa, mkazi wa Mtoni Kijichi jijini hapa, imekuwa tofauti kwani amejikuta akiyaonja maisha ya ndoa kwa saa chache na kisha kufariki, Amani linakudadavulia habari hii ya kusikitisha.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichohudhuria msiba wa binti huyo, Zai ambaye alidaiwa kuwa na ujauzito mchanga, alionekana ni mwenye siha njema hadi siku ya harusi, Jumapili iliyopita (Julai 30, mwaka huu) kabla ya kukutwa na umauti usiku wa saa 7 siku hiyo.
“Yaani marehemu alikuwa na afya njema kabisa, na siku ya harusi yake hakuonesha hata dalili zozote za kuumwa japo kuna wakati alisema anahisi kama kuishiwa nguvu.
FULL KUTABASAMU
“Muda mwingi alikuwa akitabasamu, alifurahia ndoa yake kwelikweli kama unavyojua watoto wa kike wanavyofurahia siku hiyo muhimu katika maisha yao,” kilisema chanzo hicho.
NDOA ILIFUNGWA SINZA MAPAMBANO
Kikizidi kufunguka chanzo hicho kilieleza kuwa, siku ya tukio, mumewe aliyefahamika kwa jina moja la Yasin, alifika nyumbani kwa babu wa marehemu, Mzee Msafiri anayeishi Sinza Mapambano jijini hapa na kukamilisha taratibu zote za ndoa na baada ya zoezi hilo kukamilika, Zai aliambatana na mumewe kwenda nyumbani kwao, Mtoni Kijichi.
…Hali ilivyokuwa siku ya harusi yake.
“Huwezi amini kumbe ni kama alikuwa anatuaga vile, maana tumesherehekea pale kwa nderemo na vifijo, wakaondoka zao na mumewe lakini ilipofika saa 7 usiku, tunaambiwa amefariki dunia,” kilisema chanzo hicho.
ALIANZA KUTAPIKA
Chanzo hicho kilieleza kuwa, ndugu wa karibu na marehemu walipopewa taarifa za msiba huo, walielezwa kuwa Zai alipofika nyumbani kwa mumewe, saa chache kabla ya kukata roho, alianza kutapika na mumewe akamkimbiza Hospitali ya Mbagala Zakhem lakini bahati mbaya, alifariki.
“Walifika salama salmini, wakahifadhi zawadi mbalimbali walizokuwa wamepewa na kisha kulala. Ilipofika saa saba usiku nasikia ndiyo akaanza kutapika na mumewe alipoona hali inazidi kuwa mbaya akalazimika kumkimbiza hospitalini, lakini alipofikishwa tu akafariki akiwa mikononi mwa madaktari,” kilisema chanzo hicho.
MSIBA WAWEKWA ALIPOOLEWA
Chanzo hicho kiliendelea kuweka bayana kuwa, asubuhi ya Jumatatu, Julai 31, mwaka huu, ndugu walikusanyika nyumbani kwa babu wa marehemu, Sinza-Mapambano ambapo taratibu zote za msiba ikiwemo mazishi zilifanyika pale.
“Palepale tuliposherekea harusi ndipo tulipokusanyika tena kwa ajili ya msiba. Yaani lile turubai lililotumika katika sherehe ya harusi yake ndilo hilohilo lililotumika wakati wa msiba wake, inauma sana! Tukaomboleza pale na baadaye mida kama ya saa 10 jioni, mwili wa Zai ulienda kuzikwa katika Makaburi ya Sinza,” chanzo kilizidi kueleza.
NI NDANI YA MASAA 24 TU!
Ukweli ni kwamba, mambo yote hayo yametokea harakaharaka mno, ni ndani ya saa 24 tu! Kila kitu kwenye maisha ya binti huyo kikabaki kuwa historia ya majonzi na masikitiko kwa ndugu na jamaa waliobaki duniani.
MUMEWE ABAKI NA MACHUNGU
Kwa mujibu wa chanzo hicho kilisema kikiwa makaburini hapo, mume wa marehemu alionekana kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi, haamini kwa kilichotokea, hajielewielewi kwani hata kuzungumzia undani wa mazingira ya kifo cha mkewe hakuweza.
KABLA YA NDOA ALIUMWA
Inasemekana, siku chache kabla Zai hajaolewa, aliishiwa nguvu na kukimbizwa hospitali lakini alitibiwa na kurejea nyumbani na hata ilipofika siku ya harusi, alikuwa mzima wa afya.
BABA AZUNGUMZA
Gazeti la Amani lilifanikiwa kuzungumza na baba wa marehemu, Ketel Madua ambaye alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kwa kuondokewa na binti yake huyo, saa chache baada ya kumuoezesha. Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu na jamaa kwa msiba wa Zai.
from Blogger http://ift.tt/2v3iC9e
via IFTTT