Kampuni ya Udalali ya Yono imetangaza kupiga mnada majengo matatu ya ghorofa yanayomilikiwa na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Agosti 20 mwaka huu katika gazeti la Sunday News lilitolewa tangazo la mnada wa majengo hayo ambayo ni mali ya Lugumi yanayotarajiwa kupigwa mnada Septemba 9 mwaka huu. Ghorofa moja lipo eneo la Upanga na kwa mujibu wa tangazo hilo, jengo hilo linafaa kwa ofisi na makazi, na majengo mawili ya Mbweni JKT yanafaa kwa makazi.
Scholastica Christian Kevela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono alisema kuwa miezi minne iliyopita nyuma walifungia mali za Lugumi wakimtaka alipe malimbikizo ya kodi aliyokuwa akidaiwa, lakini hadi sasa hajafanya hivyo.
Kiongozi huyo wa Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ni wakala wa serikali wa kukusanya kodi kwa wadiwa sugu ambapo hushirikiana na TRA alisema mdaiwa huyo hajalipa mabilioni ya kodi anayodaiwa na hivyo wao wamepewa amri halali ya kuzipiga mnada nyumba hizo wananzozishikilia.
Kevela alikataa kutaja kiwango cha fedha ambacho Lugumi anadaiwa na TRA akabaki akisisitiza kwamba ni mabilioni ya shilingi na kwamba TRA ndio wanajua kiwango halisi. Hata hivyo hakutangaza thamani ya majengo hayo akisema kwamba, kila mtanzania aje na fedha aliyonayo kwani wao kama madalali hawana kiwango maalum.
Aidha, Kevela aliwataka wananchi kulipa kodi bila shuruti kuepuka nyumba zao kupigwa mnada huku akisema kwamba wasipofanya hivyo na deni lao likafika kwa Yono, wao watafanya kazi yao kiukamilifu.
from Blogger http://ift.tt/2v5vAkj
via IFTTT