YULE MUUGUZI ALIYEMCHOMA MSICHANA SINDANO YA USINGIZI NA KUMBAKA ALALA LUMANDE

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia muuguzi wa kituo cha afya cha Kata ya Igulubi, Damian Mgaya (26) kwa tuhuma za kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 18 baada ya kumchoma sindano ya usingizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema muuguzi huyo ameshahojiwa na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika. Alisema msichana huyo amepatiwa fomu ya PF3 baada ya tukio hilo na jana aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake kuendelea vizuri.
“Hali ya huyu msichana imeimarika na ameruhusiwa, naye atahojiwa kwa upande wake ili tujue uhalisia wa tukio lilivyokuwa,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda huyo alisema siku ya tukio msichana huyo alifika kwenye Zahanati hiyo kumuuguza mama yake mzazi ndipo muuguzi huyo alipotumia nafasi hiyo kumchoma sindano ya usingizi kisha kumbaka.
Ntemi James, ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Igulubi amesema tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita kuanzia saa 8 usiku hadi alfajiri wakati msichana huyo akimuuguza mama yake aliyelazwa katika Zahanati hiyo.

from Blogger http://ift.tt/2u9Gyas
via IFTTT