WAZIRI WA MKAPA NA JK ATIWA MBARONI NA POLISI KWA AMRI YA MKUU WA WILAYA

Waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya tatu na nne, Dkt. Mary Nagu amekamatwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Sara Msafiri. Mbali na Nagu, wengine waliokamatwa ni Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Othman Dunga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, George Bajuta.
Viongozi hao walikamatwa jana wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa baada ya kudaiwa kuibuka vurugu kwenye kikao hicho kulikosababishwa na agenda ya uchaguzi iliyowasilishwa kwenye kikao hicho ambayo baadhi ya wajumbe hawakukubaliana nayo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na DC Sara Msafiri ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo.
Baada ya kuibuka kwa vurugu hizo, Mkuu wa Wilaya aliamuru Dkt. Mary Nagu na viongozi hao wa CCM wakamatwe na kupelekwa Kituo cha Polisi Katesh kwa ajili ya kutoa maelezo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao waliokuwa kwenye kikao cha ndani cha CCM Wilaya wakijadili masuala yao na kusababisha kuibuka vurugu zilizohatarisha usalama.
“Mkuu wa Wilaya alielekeza waende Kituo cha Polisi kutoa maelezo yao, sasa sisi tunawahoji kujua tatizo ni nini, walikuwa wanajadili nini na nani alisababisha vurugu? Kwa vile kikao hicho kilikuwa na Mwenyekiti wake, atatuambia nani walioanzisha vurugu ndani ya kikao,” alisema.
HT @ MTANZANIA

from Blogger http://ift.tt/2tpo0UX
via IFTTT