RAIS MAGUFULI APIGA TOP UTOAJI WA URAIA KWA WAKIMBIZI WA BURUNDI

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza leo tarehe 20 Julai, 2017 amefanya ziara ya Rasmi ya Kiserikali ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Ziara hiyo imefanyika katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera ambapo Mhe. Rais Nkurunziza amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake katika eneo la Lemela na baadaye mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyofanyika Mjini Ngara.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Posta ya zamani Mjini Ngara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nkurunziza kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu na nchi ya Burundi hususani katika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tanzania ni ndugu zako na Watanzania ni ndugu wa watu wa Burundi, umekuja kwa mazungumzo ya kiuchumi, tumezungumza mambo mengi ya kuimarisha biashara kati Tanzania na Burundi, katika takwimu za mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Burundi ilikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 116.5, kiwango hiki ni kidogo kwa nchi ya Burudni ambayo ina watu zaidi ya Milioni 10 na Tanzania ambayo ina watu zaidi ya Milioni 52” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Burundi na Rwanda na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Nkurunziza kuwa reli hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Nkurunziza kwa juhudi zake za kusimamia amani nchini mwake na ametoa wito kwa wakimbizi wa Burundi ambao bado wapo nchini Tanzania kuitikia wito wa Rais wao aliyewataka warudi nchini Burundi ili wakaendelee kujenga Taifa lao kwa kuwa hali ni shwari.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kusitisha utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao ili utaratibu huo usitumiwe kama kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Nkurunziza amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amesema Tanzania na Burundi ni ndugu na majirani ambao uhusiano na ushirikiano wake ulianza hata kabla ya uhuru.
Mhe. Rais Nkurunziza ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kufanya biashara Burundi na wafanyabisahara wa Burundi kuja Tanzania bila wasiwasi na amebainisha kuwa hali ya Burundi ni shwari kwani hata wakimbizi waliokimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita wameanza kurejea nchini Burundi kwa hiari yao na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Tunataka kuwajulisha wenzetu Watanzania na Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania, Burundi ya leo ni nchi yenye amani, tunawaalika Warundi wenzetu, kaka zetu na dada zetu ambao walikimbilia hapa Tanzania, warudi nchi kwao tujenge nchi yetu iwe na amani ya kudumu.
Tunapata faraja kwamba Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita ambao wanafikia idadi ya 150,000 wameanza kurudi Burundi bila ya kupitia Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), kwa hiyo tunasema wote rudini nyumbani” amesema Mhe. Rais Nkurunziza.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mawaziri watano na Mhe. Rais Nkurunziza ameongozana na Mawaziri watano ambao pamoja na viongozi wengine wa taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki mazungumzo rasmi.
Mhe. Rais Nkurunziza amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini Burundi.
Kesho tarehe 21 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kigoma ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo na barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
20 Julai, 2017

from Blogger http://ift.tt/2tlQF98
via IFTTT