Mwanamke Anayefuga Ndevu Kama Mwanaume Avunja Rekodi ya Dunia………

KATIKA umri wa miaka 25 alionao, mrembo Harnaam Kaur anashikilia rekodi ya dunia ya kuwa mwanamke mwenye nywele mwilini. Hata hivyo, ameikubali hali hiyo na kuamua kufuga ndevu, jambo linalowashangaza wengi, ikionekana ni jambo geni kwa wanawake.
Amedhihakiwa shuleni, mtaani, kazini kwake na hata katika mitandao ya kijamii, lakini kamwe hakuthubutu kuzinyoa nywele zake, akiamini Mungu alikuwa na sababu za kumfanya awe na mwonekano huo.
Ndiyo maana, leo hii ukikutana naye, ni sura na maumbile yake ya kike ndiyo yatakayokutambulisha kuwa ni mwanamke, ingawa kidevu chake kimechakaa ndevu mithili ya mwanaume, huku mdomo wake ukiwa umezungukwa pia.
Kaur ana tatizo la homoni lifahamikalo kwa Kiingereza kama polycystic ovary syndrome, ambalo humfanya mwanamke kuwa na nywele nyingi zaidi usoni. Anasema awali, wakati anaanza kuota ndevu baada ya kupevuka akiwa na umri wa miaka 11, alipata wakati mgumu shuleni na hata mtaani, akidhihakiwa, jambo lililomkera mno.
Akiwa na umri wa miaka 15, anasema kero dhidi yake zilizidi na hata kufikiria kutaka kujiua, kwani hakuyafurahia tena maisha na hata alilazimika kuwa mtoro shuleni. “Ndiyo, nilitaka kujidhuhuru kwa sababu ya hizi ndevu.
Kuna siku nilinunua vidonge vingi na kutaka kuvimeza ili nife, ulikuwa uamuzi wangu wa mwisho… lakini kama miujiza, sijui kilitokea nini sikuendelea kuwaza kujiua,” anasema Kaur, mkazi wa Slough huko Berkshire, Kusini Mashariki mwa England.
Anasema, awali alijaribu kila njia kuzinyoa nywele zilizokuwa zikiota usoni kwake. Alijaribu pia kubadilisha rangi ya ngozi, kunyoa, kutumia mafuta ya kuondoa nywele mwilini, lakini bila mafanikio. Ikafikia hatua ya kunyoa ndevu kila siku.
Lakini nywele hizo ziliendelea kuwa nyeusi na ndefu zaidi. “Nilikuwa na marafiki waliokuwa karibu nami, walinifariji lakini pia familia ilinisaidia katika wakati mgumu niliokuwa nao,” anasema. Anaongeza kuwa, baadaye alianza kujikubali na kufurahia maisha, licha ya kwamba watu wengi waliendelea kumshangaa.
Wapo pia waliotishia kumuua endapo ataendelea kuziacha ndevu zake. Na katika kuthibitisha kuwa amejikubali, Machi mwaka jana, Kaur alikuwa mwanamke wa kwanza kushiriki maonesho ya Wiki ya Mitindo London akiwa na ndevu zake, Amekuwa akishiriki pia maonesho mengine katika nchi mbalimbali.
Kwake, anasema ni heshima kubwa kwake kutambuliwa na kuwekwa kwenye Kitabu cha Rekodi za Dunia cha Guinness. Na baada ya kuacha ualimu, amekuwa mwanaharakati akipambana kuelemisha wanawake na wasichana wengine wenye matatizo ya aina yake wajiamini, kwani hawana tofauti na binadamu wengine.
“Kuna niliokosana nao kwa sababu niliamua kuachia ndevu zangu. Lakini nashukuru nimepata nguvu na sasa nataka kuionesha dunia kwamba hili ni tatizo la kawaida, watu hawapaswi kunyanyasika. “Binafsi nimegundua nina nguvu, mimi ni mrembo na mtu asiyeogopa.
Tuzo ya Guinness imenipa nguvu na ujasiri zaidi. Sasa ninajipenda kama mwanamke, ninavutia, nina marafiki na ninapata mikataba ya kazi, kimsingi maisha yanaendelea,” anasisitiza kimwana huyo ambaye amekiri kutokuwa na mahusiano kimapenzi, ingawa anaamini wakati ukifika atampata mwandani wake.
Chanzo:Habarileo
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2tyVcHP
via IFTTT