Askari wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Luhende Lusangija
**
Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Luhende Lusangija(34) mkazi mtaa wa Mwinamila Kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga amekutwa amejinyonga nyumbani kwake kutokana na kile kilichotajwa kuwa mke wake alikuwa anauza mali za familia kutokana na mikopo aliyokuwa anadaiwa.
Tukio hilo limetokea Jumamosi June 3,2017 majira ya saa 11 alfajiri ambapo marehemu akiwa na watoto wake watatu nyumbani, aliamka na kisha kuchukua mtandio huku watoto wake wakiwa wamelala, na kuamua kujitundika kitanzi sebuleni, na kusababisha kifo chake papo hapo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema mwanamme huyo amejiua kutokana na kwa kile kinachodaiwa kuwa na ugomvi wa siku nyingi na mke wake ambaye siku kabla ya tukio alikuwa ameshaukimbia mji wake.
Wakisimuliza tukio hilo majirani zake Safina Javali, alisema marehemu alikuwa na ugomvi na mkewe muda mrefu ambapo walikuwa wakipigana kila siku, kwa kile kinachodaiwa kuwa mwanamke alikuwa akikopa mikopo, na baada ya kushindwa kuirejesha alikuwa akiuza vitu vya ndani wakati mumewe akiwa safarini kwenye majukumu yake ya kikazi.
“Juzi alipokuja mwanaume kutoka safarini akakuta kitanda kimefungwa kwenda kuuzwa, ili mwanamke alipe deni la mikopo aliyokuwa akiichukua, ndipo ugomvi mkubwa ulipozuka hadi kusababisha mwanamke kuukimbia mji wake na kwenda kusiko julikana,”alisema Javali.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo kutokea walimsikia mtoto wake mkubwa wa miaka 7 majira ya saa moja asubuhi akilia kwa uchungu na kupiga kelele, kuwa baba yake amekufa kwa kujinyonga na walipofika kwenye mji huo na kuchungulia mlangoni ndipo wakamuona amenin’ginia kwenye paa la sebuleni akiwa ameshafariki.
Naye mwenye nyumba Halma Issa ambapo marehemu alikuwa mpangaji wake, alisema mji huo ulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara, na walikuwa wakiwasuluhisha lakini ugomvi wao ulikuwa pale pale, na walipopata taarifa ya kifo chake walifika eneo la tukio kasha kuwasiliana na uongozi wa mtaa ilikufuata taratibu za kisheria.
Aidha mwenyekiti wa mtaa huo wa Mwinamila Ngokolo mjini Shinyanga Yohana Munisa, alikiri kupokea taarifa za marehemu huyo majira ya saa moja asubuhi, na alipofika eneo la tukio alimkuta Lusangija akiwa tayari amejinyonga, ndipo akatoa taarifa polisi ambapo nao wakafika ili kuuchukua mwili wa marehemu.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Elias Mwita alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, huku ndugu wa marehemu wakitafutwa ili kuuchukua mwili huo kwa taratibu za mazishi.
Na Marco Maduhu-Malunde1 blog
from Blogger http://ift.tt/2qSrmhV
via IFTTT