SASA Yanga kumekucha. Baada ya kumaliza pilikapilika za kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa klabu hiyo inataka kuanza kazi ya kuunda kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao.
Kamati ya Utendaji wa Yanga imeunda kabineti ya watu watano na kuwakabidhi Sh bilioni 2 kwa ajili ya kufanya mazungumzo na nyota wao wanaomaliza mikataba mipya na kufanya usajili ili kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.
Mwenyekiti wa kabineti hiyo ni Hussein Nyika, makamu wake ni Mustapha Ulungo, huku wajumbe wakiwa ni Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa na kocha wa klabu hiyo, George Lwandamina.
Moja ya majukumu yatakayowakabili ni kuhakikisha wananasa saini za wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na klabu hiyo, ambao ni Salmin Hoza, Yusuph Ndikumana, Mbaraka Yusuph, Jamal Mwambeleko, Michael Gradiel, Raphael Daudi, Mrisho Ngassa, Youth Rostard, Said Ndemla, Ibrahim Ajib na Jonas Mkude.
Ili kupata nafasi ya kuwasajili wachezaji hao, klabu hiyo imepanga kuacha nyota wao 15, ambao hawakuwa na nafasi katika kikosi hicho na kusuka upya timu kwa ajili ya msimu ujao.
“Kamati imeazimia kusajili wachezaji wengi vijana ambao wana uwezo na wenye ubora wa kucheza Yanga na kuwaacha wachezaji 15 ambao walikuwa hawana nafasi ya kucheza, wamedhamiria kujenga timu imara yenye hadhi na mashindano ya kimataifa, ndiyo maana wametenga fungu hilo la fedha,” alisema mjumbe huyo.
Aliongeza kuwa, mbali na kufanya usajili huo wa nguvu, lakini kamati hiyo leo inatarajia kuanza mazungumzo na wachezaji Deus Kaseke, Donald Ngoma, Amis Tambwe, Haji Mwinyi, Thaban Kamusoko, Vincent Bossou na wengine ambao mikataba yao ya kuichezea timu hiyo imemalizika hivi karibuni na kupendekezwa na Kocha Lwandamina kuendelea kuwa nao.
Mmoja wa wajumbe wa kabineti hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema: “Kesho (leo) Jumatatu tutaanza kazi ya kuzungumza na wachezaji wote ambao walimalizia mikataba yao, ambao wamependekezwa kubaki na kocha Lwandamina, baada ya hapo itakuja zamu ya wachezaji wapya ambao watakuwa wameorodheshwa kwenye ripoti ya kocha wetu.”
Kwa upande wake Mkwasa, alisema Yanga ni timu kubwa na wamejipanga kufanya usajili wa nguvu wenye tija utakaowezesha kutetea ubingwa wao msimu ujao.
“Tumejipanga kila eneo ili kufanya usajili wa nguvu wenye tija ambao utazingatia vigezo vyote na mimi ndio nitaongoza jahazi hilo,” alisema Mkwasa.
Katika mipango yao ya usajili, Yanga wanadai kuwa na mpango na kuanza na beki wa kushoto wa Azam, Gadiel Michael, ili kucheza pamoja na Haji Mwinyi kwenye klabu hiyo.
Naye kiungo wa zamani wa timu hiyo, Athumani Idd ‘Chuji’, ameomba kurejea tena kundini kuvaa viatu vya Justine Zullu ‘Mkata Umeme’ na kusema uwezo wa kuitumikia timu hiyo ya Jangwani bado anao kama akipewa nafasi katika eneo la kiungo mkabaji.
“Nimeiangalia Yanga msimu uliomalizika, nimegundua bado ninao uwezo mkubwa wa kuichezea timu hiyo pamoja na umri wangu wa miaka 29, bila shaka ninaweza kulitibu tatizo la kiungo mkabaji ambalo limekuwa likiwasumbua Yanga kwa muda mrefu,” alisema ‘Pass Master’ huyo, Chuji.
Akizungumza kuhusiana na ombi hilo la Chuji kutaka kurejea tena Yanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Paulo Malume, alisema amelisikia suala hilo na atalipeleka mahali husika kwa ajili ya kulitolea maamuzi, lakini yeye hawezi kusema lolote.
“Nimelisikia suala la mchezaji huyo, kwa kifupi nitalipeleka mahala husika tuone nini watasema, kila mtu anamfahamu Chuji alikuwa ni mchezaji wetu, lakini muda mrefu umepita tangu aondoke, hivyo ngoja tuone watasemaje,” alisema Malume.
from Blogger http://ift.tt/2rLl5DT
via IFTTT