Kwa maisha ya kawaida mtaani, chipsi mayai ni moja ya vyakula vinavyopendwa na watu wengi hasa kutokana na utamu wake lakini pia ni miongoni mwa vyakula vinavyopatikana kwa haraka zaidi.
Mtanzania wa kawaida hujua kuwa Ikulu yalipo makazi na ofisi ya Rais huwa wanakula vyakula vizuri sana, hivyo ukimwambia kuwa pia wanakula chipsi mayai tena siku za sikukuu, anaweza asiamini.
Suala la kubana matumizi kama ilivyo sera ya serikali ya awamu ya tano linafanyika si tu kwa kuzuia safari za nje au mikutano kutofanyikia katika hoteli za nyota tano, ni pamoja na aina ya chakula kinacholiwa n wageni Ikulu wakati wa vikao.
Mara kadhaa tumeona viongozi wa kitaifa wakipewa pipi na juisi au wakati mwingine wakipewa sambusa wanapokuwa wanakwenda kwenye vikao au mikutano, lakini hii ya jana huenda ikawa imetia fora zaidi.
Jana Rais Magufuli aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo, kwanza licha ya kuwa siku ya mapumziko, mawaziri hao walikuwa kazini na pili, licha ya kuwa siku kama ya jana watu hula vyakula mbalimbali kama pilau, mawaziri hao waliokuwa Ikulu walikula chipsi mayai.
Ndio, umesoma sawa sawa, chipsi mayai. Si kwamba chakula hiki hakifai kuliwa na viongozi hao, au ni vibaya wao kula, lakini kwa vile walikuwa Ikulu na ilikuwa sikukuu, ungetegemea kuona wamepewa vyakula vinavyoendana na sherehe hiyo. Na hii imewashangaza wengi kwenye mitandao ya kijamii kwani ni kwa mara ya kwanza kuona viongozi wakila chipsi Ikulu.
Kutokana na fedha kuwa ngumu mtaani, nadhani ni wakati muafaka sisi wananchi tuige mtindo huu wa kubana matumizi ili tuweze kuendana na serikali hii ya Magufuli.
from Blogger http://ift.tt/2slfDUO
via IFTTT