Bunge limepitisha Muswada wa Fedha 2017 ambao unatarajiwa kuanza kutumika Julai Mosi.
Nyingi ya adhabu zilizomo kwenye muswada huo, zinatoza faini ya kati ya Sh 200,000 mpaka Sh1 milioni au kifungo kisichopungua miezi 12 mpaka miaka miwili.
Miongoni mwa makosa hayo yanahusu wachafuzi wa mazingira wakiwamo watupaji taka na wanaojisaidia mtaani. Adhabu hii ambayo awali ilikuwa Sh 50,000 au kifungo cha miezi sita, imeongezwa ili kudhibiti makosa hayo.
Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffery Michael ambaye jimbo lake linaongoza kwa kusimamia sheria zinazohusu usafi wa mazingira alitaka mabadiliko ya vifungu vingi ambavyo vinatoa adhabu kubwa au vitakuwa na athari yenye maumivu makali kwa wananchi lakini hakufanikiwa kulishawishi Bunge lililokuwa linaongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson livipunguze.
“Kwa mtazamo wangu hizo faini ni kubwa sana ukilinganisha na makosa ya wananchi wetu. Sh50,000 watu walikuwa hawawezi kulipa jimboni kwangu ambako hata kutema mate ni kosa, wengi watafungwa,” alisema Michael.
Licha ya wachafuzi wa mazingira, wamo pia wafanyabashara wadogo ambao hawatatimiza matakwa ya sheria hiyo inayotarajiwa kuanza kutekelezwa ili kufanikisha bajeti ya Serikali.
Licha ya kuwaumiza wafanyabiashara hao wenye mitaji midogo, Michael alisema kumfunga mtu wa namna hiyo kwa mwaka mmoja mpaka miwili ni muda mwingi ambao utaathiri mambo yake mengi hivyo kurudisha nyuma uchumi wa Taifa.
“Wakosaji lazima wawepo, watu wengi watafungwa na kuliongezea Taifa gharama za kuwahudumia wakiwa gerezani kwa kutafuta laki mbili au milioni moja. Naomba tuamue kwa kura,” alisema akihitimisha hoja yake.
Kura zilipopigwa, kipegele hicho kiliridhiwa. Japo mbunge mmoja alitaka kura zihesabiwe. Hilo halikutokea.
Ilikuwa ni siku ya Michael ambaye, mara kadhaa aliinuka kutaka marekebisho yafanyike kwenye baadhi ya vifungu kiasi cha kuwainua mawaziri kujibu na kufafanua hoja zake. Kwenye baadhi ya vipengele, wabunge walichangia kumuunga mkono.
Kutokana na juhudi za Rais John Magufuli kuendesha vita ya kupambana na utoroshaji wa madini nchini, alipendekeza kuongezwa kwa tozo ya ukaguzi wa madini iliyoanzishwa mwaka huu.
Akitambua uwapo wa mrabaha wa asilimia moja unaolipwa na kampuni za uchimbaji madini, alilitaka Bunge kumuunga mkono Rais kwa kuiongeza tozo hiyo ili mrabaha na ukaguzi vifikishe asilimia 10.
Kwa kuwa wizara haina waziri kwa sasa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisimama kujibu na kusema asilimia moja inatosha kwani mpaka ukaguzi huo unafanywa, “Mwekezaji atakuwa na amelipa kodi nyingine zote zilizopo kwa mjibu wa sheria.”
Kipengele kingine kilichokuwa na mvutano mkubwa hata naibu spika kulazimika kuongeza nusu saa ili kukamilisha mjadala huo, kilihusu kodi ya majengo. Mbunge huyo alitaka wajane na wasio na kipato cha hakika waongezwe kwenye kundi litakaopata msamaha.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Serikali, nyumba zote zilizopo mjini; majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya zitalazimika kulipa kodi hiyo isipokuwa zinazomilikiwa na ambazo ni makazi ya walemavu au wazee wenye zaidi ya miaka 60.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alimweleza mbunge huyo kwamba: “Wapo wajane wenye uchumi imara kuliko hata waliopo kwenye ndoa. Tukiache kipengele hiki kama kilivyo.”
Mbali ya Michael, Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Paulina Gekul aliongeza hoja ya kutaka mabadiliko ya sheria hiyo. Alimtaka naibu waziri kufahamu kuwa mara nyingi baada ya kufiwa na waume zao, wajane hunyang’anywa hata mali walizonazo.
Ni Simbachawene tena aliyemaliza mjadala huo kwa kusema: “Sheria haitakiwi kubagua. Inapaswa kuwahusu wote. Jenister Mhagama (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu), hapa ni mjane lakini anaweza kulipa kodi hii. Hakuna sheria ya namna hiyo duniani.”
Hivyo muswada huo haukuwataja wajane kwenye kundi la msamaha na pendekezo la kutaka asilimia 50 ya mapato yatokanayo na kodi hii kurudishwa halmashauri halikupata baraka za wengi waliokuwapo bungeni.
Kwa muswada huo, mamalishe, wamachinga na wachimbaji wadogo wataanza kulipa kodi. Wapo washereheshaji (MC) na watoa huduma ya chakula (caterers) ambao pia wamo kwenye orodha ya chanzo kipya cha mapato ya Serikali.
Baada ya mabishano yaliyoongozwa na Michael akiibana Serikali kufanya mabadiliko aliyoyapendekeza na baadhi ya wabunge hasa wa upinzani kumuunga mkono kuhitimishwa, muswada wenye vifungu 66 ulipitishwa na kutoa nafuu kwa shule na vyuo binafsi zilizofutiwa kodi ya SDL na tozo ya zimamoto.
from Blogger http://ift.tt/2s29FNj
via IFTTT