Hakimu Ajitoa Kusikiliza Kesi ya Godbless Lema

Hakimu Mkazi, Desderi Kamugisha, amejitoa kuendelea kusikiliza moja ya kesi za uchochezi zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).
Katika kesi hizo, Lema anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii.
Hakimu Kamugisha amejitoa katika kesi ya jinai namba 441/2016 ambayo Lema anadaiwa kutoa matamshi hayo Oktoba 23, mwaka jana wakati wa mkutano wa hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa.
“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake.
“Rais ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa Serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu wananyanyaswa,” Lema alinukuliwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Martenus Marandu.
Hakimu huyo sasa ataendelea kusikiliza kesi nyingine ya jinai namba 440/2016 ambayo pia inamhusu Lema anayedaiwa kutoa maneno ya uchochezi yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii Oktoba 22, mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro wakati wa mkutano wa hadhara.
Miongoni mwa maneno ambayo Lema anayodaiwa kuyatoa ni: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani, iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.
“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya katiba, ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”
Jana kesi hizo mbili zilipangwa kutajwa mbele ya Hakimu Kamugisha katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, lakini Wakili wa Serikali, Alice Mtenga, alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi umekamilika, hivyo wanaomba kupangiwa tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Lakini Hakimu Kamugisha alisema haoni busara kuendelea kusikiliza kesi zote wakati kuna mahakimu wengine.
“Nilikuwa na kesi nne za mshtakiwa huyu huyu, sasa zimebaki mbili. Kwangu sioni kama itakuwa busara kusikiliza kesi zote wakati kuna mahakimu wengine wanaweza wakasikiliza, najiondoa kwenye kesi namba 441, nitaendelea na kesi moja namba 440.
“Ukiangalia nature ya kesi ni ile ile moja, mshtakiwa yule yule, kwa hiyo tutaenda kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi ili apangiwe hakimu mwingine wa kusikiliza kesi hiyo ili tarehe ya kusomwa maelezo ya awali itakayopangwa, asikilize hakimu mwingine,” alisema.
Katika kesi hizo, Lema anawakilishwa na Wakili Sheck Mfinanga.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo hakuweza kufika mahakamani hapo jana kwa madai kuwa hawakuwa na taarifa za kesi hizo kupangwa.
“Nilikuwa nimesimama kwenye korido ya mahakama asubuhi nikamuona RCO, nikamuuliza kuna nini akanijibu amekuja kwenye hizi kesi, ndipo nikaamua kuja mahakamani ila Lema au wadhamini wake hawakufika,” alisema Mfinanga.
Lema alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Kamugisha Novemba 8, mwaka jana, akikabiliwa na kesi hizo.
Novemba 11, mwaka huo huo, alishindwa kupata dhamana baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kupinga uamuzi wa dhamana uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Lema alikaa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi minne kutokana na kukosa dhamana kuanzia Novemba 11 mwaka jana kabla ya kuachiwa kwa dhamana Machi 3, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

from Blogger http://ift.tt/2rQOoFC
via IFTTT