Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) afariki dunia baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au vifo.