Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe awataka bodaboda kwenda shule ndani ya miezi 2


KAMANDA  wa  polisi mkoa wa Njombe Pudensiana Protas ametoa miezi miwili kwa madereva Bodaboda mkoa wa Njombe kupata mafunzo ya udereva kabla hawajaanza kuwakamata wale watakao wabaini hawajapata mafunzo wala kuwa na reseni ikiwa ni mkakati wa kupambana na ajali zinazoweza kuzuilika zinazo sababishwa na pikipiki.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifunga mafunzo kwa madereva Bajaji na pikipiki maarufu Bodaboda 320 halmashauri ya mji Makambako ambao wamepatiwa mafunzo hayo na Taasisi ya Apec kwa muda wa wiki moja baada ya wiki iliyo pita kumaliza mafunzo hayo madereva 300 na kufikia jumla ya madereva 620.

Protas alisema kuwa anatoa miezi miwili madereva hao kupata mafunzo ili kuanza kuwasaka ambao hawana reseni za kuendesha pikipiki za mataili matatu (Bajaji) na magurudumu mawili (Bodaboda) ambao wamekuwa wakijifunza mitaani na kuingia barabarani na kusababisha ajali.

Madereva hao wametoka katika maeneo matatu tofauti ya halmashauri ya Makambako mjini na maeneo ya Pembezoni kwa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa sasa amepata waalimu zaidi ya 600 ambao watakuwa ni mabarozi na kuwaelimisha wengine kuhusiana na usalama Barabarani na anaamini walio pata mafunzo watakuwa chachu ya kupunguza ajali za barabarani.

Aidha mkurugenzi wa taasisi hiyo ya Apec, Respisius Protas ameiomba serikali kuhakikisha kuwa inawajengea vijana wa bodaboda vibanda maeneo ya kuegesha Pikipikizao ili kujiongezea kipato kama halmashauri kwa kuwa wakiwajengea maeneo ya kuegesha wataenda kuchukua ushuru hapo.

Alisema kuwa madereva hao wamekuwa wakikosa maeneo ya kuegesha vyombo vyao na wakiwa na eneo la kuegesha lina kuwa halina kibanda ambapo kipindi cha mvua hunyesewa na likiwaka jua ni lao.

Alisema kuwa kupitia mafunzo hayo madereva hao wamepata mafunzo ya ujasiliamali na uendeshaji salama wa pikipiki na kuiomba halmashauri kutenga asilimia 5 ya mapato yake kwaajili ya madereva hao kukopeshwa kwa riba nafuu.