DAR ES SALAAM, TANZANIA
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Salehe Zonga aliyekuwa amesimamishwa kwa madai ya kutumia madaraka vibaya mali za shirikisho hilo zikiwamo Sh. Milioni 15, ametoswa rasmi hivyo si kiongozi tena wa shirikisho hilo.
Januari mwaka huu, TBF ilitangaza kumsimamisha kiongozi huyo ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya Sh. Milioni 38 zilizokuwamo kwenye akaunti ya shirikisho hilo.
Ilibainika kuwa Zonga alikuwa akizitumia kinyemela kwa matumizi binafsi, madai ambayo hadi sasa katibu huyo wa zamani ameyakana.
Makamu wa Rais wa TBF, Jaffar Hamisi, alisema bodi ilikutana juzi kujadili suala hilo na kufikia uamuzi wa kumsimamisha moja kwa moja na kumpa miezi mitatu kurejesha Sh. Milioni 15.6.
“Bodi imekaa juzi na kumtaka Zonga kurudisha Sh. Milioni 15.6 ndani ya miezi mitatu. Katika kikao hicho alikuwapo na aliendelea kukataa kuwa fedha hizo hakuzitumia,” alisema Jaffar.
Jaffar, aliongeza kuwa ikipita miezi mitatu bila kufanya hivyo, TBF itamfungulia mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za shirikisho hilo.
Tuesday, March 8, 2016
Mkwasa atangaza wachezaji 25 kuivaa Chad
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Charles Boniface Mkwasa na Baraka Kizuguto Machi 8, 2016 |
TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’ imetangaza kikosi cha wachezaji 25 kitakachoivaa Chad katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), jijini N’Djamena Machi 23 mwaka huu bila kuweka kambi kama ilivyozoeleka.
Aidha Taifa Stars itawakosa Mrisho Ngassa (Free State Stars, Afrika Kusini), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga) na Aggrey Morris (Azam FC) kutokana na kuwa majeruhi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kocha wa Taifa Stars Boniface Mkwasa, alisema amewaita kutokana na kuwa sawasawa kiakili na kimwili kwa ajili ya kuwakabili Chad wanaonolewa na nyota wa zamani wa Cameroon, Rigobert Song.
“Nimewaita kwa kuwa hatuna muda wa kufanya mazoezi, ni kupanda ndege tu kwenda kuivaa Chad, mchezaji majeruhi hana nafasi kwa sasa, isipokuwa uwezo tu na utayari wa kucheza mechi hii ambayo tunataka ushindi,” alisema Mkwasa.
Mkwasa alisisitiza, “Ligi Kuu ya Vodacom, michuano ya CAF (CL, CC) inachezwa wikiendi ya tarehe 18-20 Machi, hivyo wachezaji wote watakua na majukumu katika timu zao, muda wa kufanya mazoezi kwa pamoja kwa ajili ya mchezo huo hautakuwapo, ndio maana nasisitiza wachezaji niliowachagua wahakikishe wanajilinda wenyewe kwa kuwa fit wanapokuja kwenye safari ya mchezo huo wa Machi 23.”
Wachezaji walioitwa ni magolikipa Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustapha (Yanga) na Shaban Kado (Mwadui FC), walinzi ni Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika (Azam FC) na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC).
Viungo Himid Mao (Azam FC), Ismail Juma (JKU), Jonas Mkude, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto (Simba SC), Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Farid Mussa (Azam FC), Deus Kaseke (Young Africans).
Washambuliaji ni Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), John Bocco (Azam FC), Elias Maguri (Stand United), Jeremia Mgunda (Tanzania Prisons) na Ibrahim Hajibu (Simba SC).
Katika kundi G Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama moja huku Misri ikiwa na alama sita ikifuatiwa na Nigeria yenye alama nne huku Chad ikiwa haina alama.
Baraka Kizuguto akizungumza jambo kabla ya Charles Mkwasa (kulia) hajatangaza kikosi Machi 8, 2016 |