KESI YA KUPINFGA MATOKEO YA JIMBO LA NJOMBE KUENDELEA MACHI 9



MAHAKAMA  Kuu Kanda ya Iringa imetoa uamzi wa kufanyiwa marekebisho mapungufu yaliyowekewa pingamizi na Wakili wa serikali Apimaki Mabrouk dhidi ya mlalamikaji Emmanuel Masonga katika kesi ya uchaguzi inayowakabili Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Edward Mwalongo, Msimamizi wa Uchaguzi wa wa jimbo hilo Eliminata Mwenda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akitoa uamzi huo katika ukumbi wa mahakama hiyo mjini Njombe, Jaji Jacob Mwambegele, amesema pamoja na kukubaliana pingamizi liliowekwa na wakili wa serikali Mabrouk kwamba katika ombi la kesi hiyo aya 7,8,9 na 10 zinamapungufu kisheria kutokana na maelezo yake kutojitosheleza, lakini hakubaliani na ombi lake la kutaka kuzifuta ili shauri hilo liondolewe mahakamani.

Badala ya kuzifuta aya hizo Jaji Mwambegele, ametoa siku saba  kwa mlalamikaji katika kesi hiyo Masonga, ambaye alikuwa mgombea wa ubunge wa Chadema katika jimbo hilo kufanyia marekebisho, na kwamba akishindwa ndani ya muda huo, kesi hiyo itafutwa na atatakiwa kulipa gharama zote.

Awali Machi mosi, mwaka huu Wakili wa serikali Apimaki Mabrouk aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali hati ya shauri ya kesi hiyo kwa kile alichodai kuwa hoja za mlalamikaji katika hati yake ya maombi katika aya 7, 8, 9 na 10, zina maelezo yasiyojitosheleza hivyo itakuwa ngumu kwa upande wa walalamikiwa kujitetea, na kwamba hatua hiyo itasababisha kesi hiyo kuchukua muda mrefu hadi kutolewa uamzi.

Mara baada ya uamzi huo nje ya Ukumbi wa mahakama Wakali wa Masonga, Edwin Swale amesema watafanya marekebisho ndani ya muda uliotolewa na mahakama ili kesi iweze kuendelea machi 16 mwaka huu.