'UKEKETAJI' Mfumo jike unaoendekeza mfumo dume



Na Gordon Kalulunga.

KWA mujibu waWIKIPEDIA, kamusi huru, inaeleza kuwa Ukeketaji ni neno linalotokana na mzizikeket, ambao unabeba maana ya kuharibu. 
 
Mara nyingi tendo laukeketaji unaitwa pia "tohara" kwa kulifananisha na upasuaji mdogo wa wanaume lakini mambo ni tofauti kabisa.

Hapa sehemu za nje za viungo vya uzazi zinakatwa kusudi wasifurahie sna tendo la ndoa, hivyo wawe waaminifu zaidi kwa waume wao.

Kinyume na tohara ya wavulana matabibu wanaona hasara nyingi katika desturi hiyo. Ukeketaji unasababisha wasichana wengi kufa na wengine wengi kupatwa na maumivu makali wakati wa hedgi, wa tendo la ndoa na wakati wa kujifungua.

Kwa sababu hizo serikali nyingi za dunia zimeupiga marufuku. Pia madhehebu kadhaa yanatoa mafundisho kuwa ni kinyume cha masharti ya dini yao.


Kila mwaka ifikapo Februari 9, hapa nchini tunaanzimisha siku ya kupinga ukeketaji. Leo hii tunajitahidi kama nchi kupinga vikali vitendo tulivyovipachika jina la ukatili wa kijinsia ama wengine wanaita majina kadha wa kadha likiwemo jina la mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Mambo haya yanapingwa zaidi na watu waliopo mijini, lakini wale waliopo vijijini kwao hali zile ni za kawaida sana na  kizuri au kibaya hata watu waliopo serikalini wanaungana na baadhi ya watu wa vijijini kwao hususani katika suala la ukeketaji.
 
Mwaka 2012-12013, nikiwa chini ya mpango wa fellowship chini ya mfuko wa kusaidia vyombo vya habari nchini Tanzania Media Fund(TMF), nikibobea katika uandishi wa afya ya uzazi, nilifika mkoani Mara katika wilaya za Bunda, Butiama na Musoma na kubaini mamboi kadhaa.
Baada ya serikali kuonekana kuzuia na kukataza mila ya baadhi ya makabila hapa nchini kuwakeketa wasichana, mkoani Mara, baadhi ya makabila yanayokeketa yamebuni mbinu mpya.
 
Mbinu inayotumika kwa sasa kuwakekata wasichana hao ni kuandaa sherehe inayofanana na siku ya kuzaliwa yaani(Birthday).
 
Baadhi ya wananchi na viongozi wa afya wilayani Musoma na Bunda mkoani Mara walioomba hifadhi ya majina yao, wanasema bado ukeketaji unandelea kufanyika kwa wasichana hasa nyakati shule zikifungwa.
Wanasema mbinu inayotumika ili kukwepa mkono wa sheria kwa wakeketaji ni kuwakusanya mabinti wachache au mmoja mmoja na kuwakeketa huku wakiimba nyimbo za kumpongeza binti kwa kuazimisha siku yake ya kuzaliwa.
‘’Mbinu inayotumika kwasasa na vifaa vya mangariba ni vile vile, lakini ilikukwepa mkono wa sheria na kukamatwa wazazi wa wasichana na mangariba hao, hupanga mbinu nzito na baada ya kuwakeketa wasichana hao uimba wimbo wa Happy birthday’’ walisema kwa nyakati tofauti wananchi hao.
Baadhi ya wasichana wanaoishi wilayani Musoma waliohojiwa na mwandishi, walisema wao tayari wamekeketwa na hawaoni ubaya wa kitendo hicho kwasababu ndiyo mila na desturi za makabila yao.
 
‘’Ni kawaida tu, mbona hata wanaume wanaenda jando! Tatizo labda ni kwamba ninapotaka kukutana kimwili na mtua siye wa kabila la kwetu huwa naona aibu kidogo maana hata nikienda nae mimi nachelewa kufika kileleni wakati yeye anawahi na hisia zangu zinakuwa mbali’’ alisema ‘’Judith’’ jina siyo halisi.
 
Dhana hiyo ya kukeketa baadhi ya makabila yanaamini kuwa kukeketa kutalinda ubikira wa wasichana na kuwafanya wanawake wasiwe wahuni (Malaya).
Pia wapo watu wengine wanaamini kwamba kumkeketa msichana ni heshima kwa mwanamke.
 
Baadhi wanasema hali hiyo inaongeza raha ya kujamiiana kwa waume zao, na kitendo hiki kinaaminika kuongeza uwezekano wa wanawake kuolewa na kuimarisha uwezo wa kuzaa.
 
Madhara yake ni nini?
Wataalam wanasema kuwa kukata sehemu za via vya uzazi kunaweza kusababisha kutoka damu nyingi. Hii inaweza kusababisha kifo au upungufu mkubwa wa damu kwa mkeketwaji hatimaye kufariki dunia.
 

Maambukizi ya magonjwa.
Mambukizi ya magonjwa ya naweza kutokea kwasababu ya kutumia vifaa vichafu na pia yanaweza kutokea kwa kutumia dawa za kienyeji za kuponyesha vidonda.
Maambukizi yanaweza yakaenea hadi kwenye tumbo la uzazi, mirija ya kupitishia mayai, na kwenye mayai ya uzazi na kusababisha maumivu ya mara kwa mara hata ugumba. Mambukizi ya magonjwa yanaweza kusababisha kifo.
 
Kubana mkojo:
Baada ya kukeketwa wanawake wanaweza kubana mkojo kwasaa nyingi au siku nzima kwasababu ya maumivu au kwa kuogopa kupitisha mkojo kwenye vidonda. 
 
Hata baada ya vidonda kupona mwanamke aliyeshonwa uke, tundu linaweza likawa dogo mno kuweza kutoa mkojo.
 
Matatizo wakati wa siku za hedhi:
Kama mlango wa uke ni mdogo sana kiasi cha kutoruhusu damu ya hedhi kutoka vizuri, damu inaweza kukusanyika ndani ya uke na tumbo la uzazi.
Hii inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa, na tumbo la uzazi kuvimba kwasababu ya damu ya  hedhi.
 
Ushauri;
Jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu ubaya wa kitendo hicho cha ukeketaji kabla ya kutumia nguvu, maana katika jamii ya wanaokeketwa inaamini kuwa hakuna mwanamke anayeweza kuolewa bila kukeketwa.

Lakini tujiulize kuwa je nani anaendeleza mfumo dume katika jambo hili? Jibu linaweza kuwa ni kwamba, wanawake wanaendeleza mfumo jike kwa kuutukuza mfumo dume.
Maswali yafuatayo ni vema yakajulikana vizuri kuwa, Je wanawake hawawezi kuolewa bila kukeketwa? Je wanawake wakikataa kukeketwa wanaume hawatawaoa?
Basi cha kufanya ili kufanikiwa katika suala la ukeketaji wa wanawake, ukemewe kwa nguvu zote za jamii, kuwaeleza wanawake wanaoendekeza mila hiyo ambayo tafsiri yake ni mfumo jike kuendekeza mfumo dume.
Mwandishi 0754 440740
kalulunga2006@gmail.com