MBEYA KILA JUMAMOSI SIKU YA USAFI NI KUTOKANA NA AGIZO LA RAIS DR. MAGUFULI


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Rais.


Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Mbeya, Stellah Kategile akisoma taarifa ya utekelezaji wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kwa Mkoa wa Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro akimkabidhi boksi la dawa kwa ajili ya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU Mganga mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina kwa ajili ya kuzisambaza kwa watumiaji.


Baadhi ya madawa na vifaa mbali mbali vilivyonunuliwa kutokana na gharama za maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani zilizokuwa zifanyike kimkoa Wilaya ya Mbarali zikiwa kuokolewa

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya


KATIKA kutekeleza agizo la Rais kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani na Uhuru wa Tanzania Bara, Mkoa wa Mbeya umetenga siku ya kila jumamosi kuwa siku ya usafi endelevu na kununuamadawa  ya magonjwa nyemelezi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema katika maadhimisho yaliyofanyika Disemba mosi mwaka huu kuna shughuli nyingi zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na ununzi wa madawa, utoaji wa elimu na shughuli za kijamii.

Kandoro alisema jumla ya madawa yenye thamani ya shilingi Milion 3,550,000 yamenunuliwa na kukabidhiwa kwa Mganga mkuu wa Mkoa ambaye atasambaza katika Zahanati, Vituo vya Afya na Mahospitali yanayotoa huduma.

Alisema maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo yalikuwa yafanyike Wilayani Mbarali kimkoa yalianza Novemba 13 mwaka huu kabla ya maagizo ya Rais kutolewa ambapo wadau zaidi ya 50 walijitokeza na kuchangia fedha pamoja na vifaa mbali mbali vyenye thamani ya shilingi Milioni 32.

Alisema vifaa vilivyotolewa kuwa ni pamoja na Mipira, sare za mpira, mafuta ya gari, vipeperushi,Kondomu, vikombe, kofia, T shirt, Ndoo na Kanga ambavyo vyote watapewa walingwa ambao ni Watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya ukimwi.

Alisema shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuendesha midahalo ya wazi katika jamii kuhusu kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi katika Kata za Igulusi, Chimala, Mapogoro,Rujewa na Ubaruku katika Wilaya ya Mbarali.

Aliongeza kuwa shughuli zingine ni pamoja na kuendesha mashindano mbali mbali ya mpira wa miguu, kutoa mafunzo kwa waelimisha rika, Semina, Ushauri nasaha na upimaji pamoja na kutembelea klabu za watoto wanaoishi na VVU.

Kuhusu maadhimisho ya sherehe ya miaka 54 ya Tanzania Bara Kandoro alisema Mkoa wa Mbeya umeanza kutekeleza agizo la Rais la kuitumia siku hiyo kufanya usafi ambapo katika kikao cha viongozi wa Wilaya zote walikubaliana kuanza utekelezaji Disema 2 mwaka huu kwa kila Halmashauri kutenga siku ya kufanya usafi.

Alisema mbali na kuanza tarehe mbili pia waliazimia kutenga siku ya Jumamosi ya kila wiki kuwa ni siku ya usafi ili kujenga tabia ya wananchi kuuchukia uchafu na kupenda usafi ili zoezi hilo kuwa endelevu.

Alisema siku ya kilele ya Disemba 9 kila mwananchi kuanzia ngazi ya Kaya hadi Halmashauri bila kujali nafasi aliyonayo anapaswa kujitokeza kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka kwa kuhakikisha mifereji na mitaro inazibuliwa.

Alisema kuna changamoto ya vifaa vya kuzibulia mifereji pamoja na usombaji wa taka ambapo ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha wanapata vifaa hivyo ikiwa ni kwa kukodi ama kuazima ili mradi zoezi lifanyika kwa kiwango kizuri.