Wakati wapenzi, wafuasi, wanachama, viongozi na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na wengine wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa ujumla, wakijiandaa kutoa heshima za mwisho kwa Kamanda Alphonce Mawazo aliyeuwawa kikatili mwishoni mwa juma lililopita akiwa anatekeleza majukumu yake ya kisiasa kama Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita, tayari viongozi waandamizi wa chama na wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni, wameanza kuwasili jijini Mwanza kushiriki msiba huo mzito.
Mwenyekiti wa Chama Taifa Freeman Mbowe akiambatana na Mgombea Urais Edward Lowassa, Wakurugenzi wa Chama Taifa na Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni, wameshawasili jijini Mwanza wakitokea Dodoma.
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye pia amewasili jijini humo tangu asubuhi leo.
Viongozi hao wamekuja jijini Mwanza kuungana na Watanzania wengine kuomboleza na kujiandaa kutoa heshima zao za mwisho kwa Kamanda Mawazo ambaye anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Chikobe, wilayani Geita.
Baada ya viongozi hao kuwasili na kupewa taarifa za awali kuhusu maandalizi ya ratiba ya utoaji wa heshima za mwisho kwa Kamanda Mawazo, wamesikitishwa sana na kitendo cha Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kuzuia shughuli hiyo kufanyika jijini humo katika eneo lolote lile, ikiwemo Ofisi za CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi zilizoko jijini Mwanza.
Itakumbukwa kuwa CHADEMA kupitia uongozi wa Kanda ya Ziwa Magharibi, ilipanga ratiba ya kumuaga Mawazo kuanzia jijini Mwanza kisha mjini Geita kabla ya kuzikwa kijijini kwao Chikobe.
Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Geita, Mawazo pia alikuwa Kiongozi wa Kanda hiyo ambayo inajumuisha mikoa ya Kagera, Mwanza na Geita.
Baada ya Jeshi la Polisi kuzuia heshima za mwisho kumuaga Mawazo zisifanyike Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza kama ilivyopangwa na CHADEMA, lilikubali shughuli hiyo ifanyike uwanja wa ofisi hiyo kabla ya baadae tena kuzuia.
Viongozi hao waandamizi kwa sasa wanaendelea na kikao, taarifa za kina zitatolewa baadae.
Taarifa zaidi za ratiba na utaratibu wa kuaga mwili wa Kamanda Mawazo kwa kumpatia heshima zote zinazomstahili kama mmoja wa wapiganaji mahiri na makini, aliyejitoa kwa ajili ya MABADILIKO ya kweli kwa ajili ya Watanzania wanyonge, kabla maisha yake hayajakatishwa kikatili, zitaendelea kutolewa kadri itakavyotakiwa.
Katika hatua ya sasa, chama kinaendelea kusisitiza kauli ya Mwenyekiti wa Chama ya kuvitaka Vyombo vya Dola, kumaliza sintofahamu kubwa iliyopo kuhusu kifo cha Kamanda Mawazo hususan kutoa taarifa kamili ya unyama huo na kuwakamata wahusika wote walioratibu na kutekeleza uovu huo wa kumuua Mawazo kikatili mchana kweupe na viwafikishe kwenye mikono ya sheria mara moja.
Imetolewa leo Jumamosi, Novemba 21, 2015 na;
Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
CHADEMA