Katika kuunga mkono juhudi za serikali za kupanua wigo wa elimu Tanzania, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imetoa ufadhili kwa wanafunzi wahitaji katika masomo ya chuo kikuu.
Wanafunzi hao waliofaulu daraja la kwanza wanaanza masomo yao mwaka huu wa masomo katika chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Wanafunzi waliopata ufadhili huo ni Michael Daniel na Consolatha Mushi wanaokwenda kusomea uhandisi wa ujenzi na Lisa Kalokola anayekwenda kusomea uhandisi wa madini katika chuo hicho.
Ufadhili huo utahusisha gharama za karo, malazi na fedha ya kujikimu kwa mwezi kwa asilimia 100. Meneja Miradi Endelevu wa SBL, Bi. Hawa Ladha amesema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa ufadhili huo unafanyika kupitia mfuko wa East African Breweries Limited (EABL) Foundation.
“Hii ni moja ya mikakati ya kampuni hii kusaidia jamii,” alisema.
Alisema mfuko huo hutenga fedha kila mwaka kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ya elimu. Alifafanua kuwa wanafunzi waliopata ufadhili huo ni wale walioomba na kutimiza vigezo vilivyowekwa na kampuni.
Aliwataka vijana hao kutumia vizuri ufadhili huo kwa kusoma kwa bidii ili baada ya kuhitimu waweze kutoa mchango kwa familia zao na taifa kwa ujumla. Mmoja wa wanafunzi hao, Bw. Laurent alisema ufadhili huo utamsaidia sana katika masomo yake.
“Nimefaulu vizuri kidato cha sita lakini sikuwa na uwezo, ufadhili huu wa asilimia 100 ni ukombozi,” alisema. Alisema atatumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri ili ndoto zake katika maisha zitimie. Naye Bi. Kalokola alikipongeza kiwanda hicho kwa kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia jamii na hasa katika sekta ya elimu.
“Wanafunzi wasio na uwezo wachangamkie fursa kama hizi zinapotangazwa,” alisema. EABL Foundation imeanza kutoa ufadhili huo wa elimu vyuo vikuu tangu mwaka 2005 na kufaidisha zaidi ya vijana 200 katika nchi za Afrika ya Mashariki. Kwa Tanzania, programu hiyo imeshafadhili vijana zaidi ya 25 wanaofanya kazi katika kampuni mbalimbali.
Meneja Miradi Endelevu wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bi. Hawa Ladha akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuhusiana na ufadhili uliotolewa na kampuni hiyo kwa vijana watatu katika masomo yao Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ufadhili huo wa asilimia 100 unafanyika kupitia mfuko wa East African Breweries Limited (EABL) Foundation.
Meneja Miradi Endelevu wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bi. Hawa Ladha (wa pili kulia) akimpongeza mmoja wa wanafunzi waliofanikiwa kupata ufadhili wa kampuni hiyo kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka huu wa masomo, Michael Patrick mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Wengine ni wanafunzi waliofaidika pia na ufadhili huo, Consolatha Mushi (kushoto) na Lissa Kalokola (wa pili kushoto). Ufadhili huo wa asilimia 100 unafanyika kupitia mfuko wa East African Breweries Limited (EABL) Foundation.