Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Flava, Luteni Karama (kushoto), amefanya ujio mpya wa kimuziki baada ya kuachia ngoma moja kali iitwayo ‘The Way I Feel’ akimshirikisha msanii toka Ufaransa, Jerry Julian (chini) na tayari imeanza kufanya vema kwenye mitandao na vituo vya redio na runinga.
Karama amepasha kuwa, baada ya kimya kirefu, ameamua kurejea kwenye game kwa mtindo tofauti ambapo muelekeo wake unathibitika katika kazi yake mpya ya The Way I Feel ambayo tayari imeshapakuliwa mara laki moja na ushee tangu aiachie rasmi wiki tatu zilizopita.
“Nimeamua kuja kivingine. Si unajua siku hizi game imebadilika sana. Lazima ujiongeze na kuangalia mwelekeo kabla hujafanya chochote, ndio maana nikaamua kumshirikisha Jerry Julian ambaye kishafanya kazi kwenye majukwaa makubwa ya Ulaya kama Paris, Amsterdam, London na Marekani ya Kusini. Ukifungua Youtube utaiona na utabaini ninamaanisha nini,” akasema Karama.
Msanii huyu aliyezikoga sifa kedekede akiwa na kundi la Gangwe Mobb akiwa na mwenzake Inspektah Haroun, amesema kuwa, wimbo wake huo umerekodiwa Natal Studio hapa nchini huku ukifanyiwa mixing nchini Ufaransa na studio ya 20K Records kisha mastering ikafanywa na Macles Studio ya Ubelgiji ambayo wanamuziki wengi wa Reggae na Dancehall hufanyia kazi zao.
“Kwa kweli this time around sijabahatisha, ninamaanisha ninachokifanya nan i mwanzo wa mfululizo wa kazi nzuri siku za usoni. The Way I Feel imebeba mseto wa Bongo Flava na mirindimo ya ki-Caribbean na baada ya kuachia kazi zingine tano nilizoandaa na wasanii mbalimbali nitafanya ziara ya mataifa mbalimbali kwa mujibu wa ratiba yangu,” akasema kwa kujinasibu.
Tayari wimbo huo umepata wasikilizaji wengi mitandaoni huku wengine wakiupakua (downloading) kutoka mitandao ya YouTube, Facebook na blogu mbalimbali maarufu kote nchini na baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, hatua ambayo Karama anadai inachagizwa na ubora wa video yake iliyotengezwa na Minzi Mims wa Fine Image ya jijini Dar es Salaam.