DSC05590
Mmoja wa wanufaikaji wa mradi wa kunusuru kaya maskini mkazi wa kijiji cha Mwanga tarafa ya Nduguti wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Agnes Samson,akionyesha mradi wa Mbuzi aliouanzisha kwa fedha za TASAF. Nyuma yake ni Mratibu wa TASAF wilaya ya Mkalama, Athumani Jumanne Dulle.
Watanzania wamekuwa wakipambana kila siku  ili kijikwamua kutoka katika umasikini uliokithili wa kukosa hata milo mitatu na mahitaji muhimu kama afya , maji , malazi , mavazi na elimu. Serikali  ya awamu ya nne ikiongozwa na Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ilipambana  vilivyo kuhakikisha inasaidia watanzania hasa wale walioko katika kaya masikini sana  Tanzania kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kujikwamua katika hilo.
TASAF ni Mfuko wa Jamii, ambao Serikali inausimamia na kuutengea fedha pamoja na kupata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo, miongoni mwa wadauwa maendeleo ni Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani (USAID) na Serikali ya Uhispania (Spain)
Mufuko wa maendeleo ya jamii(TASAF) umeanzishwa kwa dhumuni la kufadhili na kuwezesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo nchini Tanzania. Makala hii imejikita katika kuchanganua  na kuelezea kwa jinsi gani mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ulivyosaidia kaya masikini Tanzania.
Lengo kuu la mfuko huu ni kuwezesha jamii zenye kipato cha chini kuinua hali yao ya  kimaisha  kwa kuanzisha shughuli zitakazo inua uchumi wao kwa kupitia taasisi zao wenyewe. Taasisi hizi zitaundwa na wao wenyewe kwa kuanzia ngazi ya kikundi na hatimae vikundi vitaunda jumuiya na hata kuunda shirikisho la kuwakomboa wao wenyewe.
Malengo  mahususi ni  pamoja  na  kuwezesha  uundaji  wa  hiari wa vikundi vyenye  mwelekeo  mmoja na kuanzisha  ushirikiano baina ya vikundi na taasisi zingine za maendeleo ili kukuza mitaji, stadi za kazi na ujuzi, Kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba miongoni mwao, Kuwezesha vikundi vyenye ari vya watu maskini kutekeleza shughuli za kuzalisha mali, kusaidia shughuli za uwekezaji kwenye miradi midogomidogo inayotekelezwa na watu maskini ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na Kujenga uwezo wa wanakikundi na taasisi zao za kijamii, kama vile  Halmashauri za vijiji nk.
Mfuko huu umekuwa na awamu kuu tatu  mpaka sasa za kuwezesha kaya masikini Tanzania kujikwamua kiuchumi. Baada ya kukamilika kwaAwamu ya I na ya II , TASAF imeleta  mafanikio makubwa kwa pande zote mbili za nchi yetu ya Tanzania ( Zanzibar na Tanzania Bara.) kwa kuwa  jamii maskini zimewezeshwa kutekeleza miradi zaidi ya13,954 ( kawa awamu ya Kwanza miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni 1,704 na wakati wa Awamu ya Pili jumla ya miradi 12,250 ilikamilika).
Mpango  wa TASAF unaotekelezwa  katika  Halmashuri  za wilaya  zote nchini  na uwemezesha utekelezaji wa Mpango wa Jamii na Uhawilishaji Fedha  kwa  kaya  maskini ambapo kaya maskini sasa 12,665 zenye  walengwa 25,782 zilifikiwa na kufaidika kutokana na utekelezaji wa Mpango huu kwa kuwekeza  katika  lishe, afya na elimu ili kujikwamua katika umaskini. TASAF pia ilihamasisha na kujenga uwezo wa jamii kwa kuunda vikundi 1,778 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye jumla ya wanachama 21,712.
Katika  uzinduzi  wa awamu ya tatu ya mpango wa maendeleo wa (TASAF) Agosti ,15 , 2012 mjini Dodoma Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete alisema utekelezaji wa Awamu ya Pili ya TASAF ulikuwa na mafanikio makubwa na  jumla ya miradi 11,572 imetekelezwa na kati ya hiyo,  miradi  4,294  ilikuwa ya huduma za jamii;  miradi 1,405 ya ujenzi  na miradi 5,875 ya makundi maalum. Miradi hiyo imegharimiwa na serikali kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo.
“Serikali imetoa Shillingi bilioni 32.2 na Benki ya Dunia ilitupatia mkopo wa masharti nafuu wa Shilingi bilioni 322. Washirika wetu wengine walituongezea nguvu kwa kuchangia Shillingi bilioni 72. Aidha, wananchi wametoa fedha, rasilimali na nguvu kazi ambazo thamani yake inakadiriwa kuwakwa ujumla ni  zaidi ya Shilingi billioni 20.2.”  Rais mastaafu Dktr jakaya Kikwete alifafanua.
 
katika uzinduzi huo Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amesema miradi ya Huduma za Jamii imeongeza na/au kuboresha madarasa 5,485; ofisi za walimu 150;  nyumba za walimu 152;, maabara kwenye shule za sekondari 157; majengo ya utawala katika shule za sekondari 20; mabweni ya wanafunzi 163; vyoo vya wanafunzi 705; madawati 22,946, viti 5,483, meza 4,354; vituo vya afya 63; zahanati 606,  nyumba za watumishi wa zahanati 301, vyoo kwenye zahanati 339, vichomea taka 182; vituo vya maji 2,198, visima virefu 192, visima vifupi 335 na matanki ya maji 205.
DSC05594
Familia Yeremia Lyanga, wakazi wa kijiji cha Mwanga wilaya ya Mkalama wakiwa nje ya nyumba yao mpya walioijenga kwa kutumia fedha za TASAF.(Picha zote na Nathaniel Limu).
kwa upande wa miradi ya ujenzi, yenyewe imeongeza au kuboresha barabara za vijijini 825; mabwawa madogo 78; mifumo midogo ya umwagiliaji 289; mifumo ya kuondoa maji ya mvua barabarani mita 4,593; maghala ya kuhifadhia nafaka 113; masoko 80; makaravati 901; madaraja ya watembea kwa miguu 64; na, miradi ya mazingira 608 yenye walengwa 566,938.
Na miradi ya makundi maalum imetoa huduma kwa yatima 32,113; wajane 15,205; wazee 17,961; watu wenye ulemavu 7,840; watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI 52,316; na vijana wasio na ajira 36,859.  Vilevile, watu 2,083 wamehamasishwa kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI.
Mafanikio ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya TASAF  hayakuishia hapo. Vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 vimeundwa kupitia Mpango wa Kuweka Akiba na Kuwekeza (COMSIP) katika Halmashauri 44 zilizopo Tanzania Bara, Unguja na Pemba. Walengwa wote wamepatiwa mafunzo ya kuendesha vikundi vyao kwa ufanisi pamoja na vifaa. Vilevile, mafunzo ya usimamizi, utekelezaji bora wa miradi na fani mbalimbali katika ngazi ya vijiji, wilaya na Taifa yametolewa kwa walengwa 27,373.
Serikali kupitia TASAF imefanikiwa pia kutekeleza Programu ya Kijamii ya Uhawilishaji Fedha kwa Kaya Maskini kwa majaribio katika Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Chamwino. Walengwa zaidi ya 13,000 kutoka kaya 6,000 maskini na zilizo katika mazingira hatarishi zilipatiwa ruzuku ya jumla ya shillingi bilioni moja na nusu.   Kaya hizo zimejengewa uwezo na watoto sasa wanapelekwa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa ajili ya chanjo na kufuatiliwa maendeleo yao.
Aidha TASAF imewezesha watoto 1,638 ambao hawakuweza kwenda shule kwa sababu ya umasikini sasa wameandikishwa na wanakwenda shule,kati ya wanafunzi hao, 392 wamefaulu kwenda shule za sekondari za kata. Vile vile wazee 4,956 wamewezeshwa kupata huduma za afya na baadhi yao wamejiunga na bima ya afya ili kupata huduma kwa urahisi na uhakika zaidi.  Kufuatia mafanikio ya haraka ya programu hii, sasa maandalizi yanafanyika ili isambazwe kwenye Halmashauri zote katika utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya TASAF.
“Katika miradi yote kwa awamu tatu changamoto  kubwa iliyojitokeza ilikuwa uhaba wa fedha za kukidhi mahitaji makubwa ya maombi ya miradi na jumla ya maombi ya miradi 110,000 iliwasilishwa TASAF na kati ya hiyo iliyotekelezwa ni 13,954,kutokana na changamoto hizo Serikali yangu ya awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imepambana kupata fedha  ili kuwezesha miradi mbalimbali” alisema Rais Mstaafu  Mhe Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, wakati akizindua wa mradi wa TASAF awamu ya tatu uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2012 huko Dodoma.
Pamoja na changamoto zilizojitokeza, Mhe. Rais alionyesha kuridhishwa kwake na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Awamu mbili za TASAF zilizotangulia na akaagiza Awamu ya Tatu ya TASAF iendeleze yale mazuri yote yaliyopatikana pamoja na kuongeza ubunifu wa jinsi watakavyoweza kuwatambua walengwa wa mpango huu.
Serikali  imeendelea  na jitihada  za kupunguza umaskini kwa kusimamia utekelezaji wa Awamu ya II na III ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Awamu ya II pamoja na mambo mengine, ililenga kuhamasisha jamii yenye kipato cha chini kujiwekea akiba na kuwekeza. Kupitia Mpango huo, jumla ya vikundi 1,620 vyenye wanachama 20,869 kwa upande wa Tanzania Bara na vikundi 158 vyenye wanachama 1,843 Zanzibar viliundwa na kupewa mafunzo na hivyo kuwekeza. Hadi kufikia Juni 2013, vikundi hivyo viliweza kuweka akiba ya Shilingi milioni 710. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 499 zilikuwa zimetolewa kama mikopo nafuu kwa wanachama. Kiwango cha marejesho ya mikopo hiyo kilikuwa ni asilimia 76.
Katika Awamu ya III ya TASAF, Serikali pamoja na mambo mengine imelenga kuhawilisha fedha kwa kaya maskini kwa masharti ya kaya hizo kupeleka watoto shule na watoto wadogo wa chini ya miaka 5 kupelekwa kliniki. Kupitia Mpango huo, kaya maskini 580,844 zimetambuliwa nchini na 436,275 zimeandikishwa kwenye Mpango. Kati ya kaya zilizoandikishwa, kaya 260,173 zimewezeshwa jumla ya Shilingi bilioni 33.3. Uhawilishaji unaendelea katika maeneo mengine kwa mujibu wa  Kalenda ya Malipo ya kila baada ya miezi miwili.
Mmoja kati ya wananchi walionufaika na mfuko wamaendeleo ya jamii TASAF Bi mwajabu Mpoma kutoka wilaya ya Mahenge mkoani Morogoro TASAF imemwezesha kupata ruzuku iliyomsaidia kuboresha maisha yake na kuishukuru TASAF kwa kutoa  ruzukuya fedha kwa kaya hivyo kunufaika kiuchumi.
 kilichobaki ni utekelezaji wa kile kilichopo kwa mfuko huu kuwezesha jamii nyingi zaidi masikini Tanzania ili kupunguza wimbi la vijana  na watoto wengi kukimbilia mjini bila kujua wanakuja kufanya nini mjini. Wawape uwezo wa kufanya maendeleo yao wakiwa katika mazingira yao na sio kusema kuwa maendeleo yako mjini hasa majiji maarufu kama Da es saalaam ,Arusha , Mbeya, Mwanza, na Tanga bali maendeleo ni kufanya kazi kwa bidii za uzalishaji mali na kuwajibika katika ufanyaji kazi wako.
Waswahili wanasema myonge mnyongeni ila haki mpeni kwa awamu ya nne kwa miaka kumi(10) iliyopita chini ya Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete imewezesha wananchi kujikwamua kiuchumi zaidi kupitia sera na utekelezaji wake katika  sekta tofauti kwa kuwawezesha wanachi wa hali ya chini hasa walioko vijijini kujikwamua kiuchumi kwa kufanya uzalishaji mali weye tija kwa kuwapo kwa mazingira mazuri kama vile mitaji vifaa na masoko ya kutosha kwa bidhaa zizalishwazo.
Katika kusherekea miaka 54 ya uhuru wa  Tanzania na kumalizika kwa awamu ya nne ya serikali  ya Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete watanzania tumeachiwa nyenzo kubwa ya kujikwamua kichumi hasa kwa zile kaya masikini nchini. Mfuko wa maemdeleo ya jamii( TASAF) umeleta mwanga wa mafanikio zaidi hata kwa serikali mpya ya awamu ya tano chini ya Mhe Dkt John Pombe Joseph Magufuli kuendeleza mfuko huo kwa kuwezesha miradi zaidi kuratibiwa na kutekelezwa chini ya mfuko huo ili kufikia malengo ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu.
TASAF imeibua na kuendeleza harakati za serikali za kupambana dhidi ya umasikini na kupunguza umaskini kwa kuzifikia jamii zilizoko vijijini zaidi na zenye mahitaji na changamoto hasi katika kupambana na umasikini katika kaya na jamii zao. 
Kujikwamua kutoka katika umasikini sio jukumu la serikali pekee bali la kila mwananchi wa nchi hii kama kweli tunataka kujikwamua katika hili basi tuwe wakweli kwa nafsi na nchi yetu kwa kuwajibika katika sehemu zetu za kazi ili kuleta kasi ya mabadiliko ya kiutendaji na kuleta mafanikio ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kiujumla. Tudumishe na kuendeleza mazuri yote yaliachwa na serikali za awamu zote ndani ya miaka 54 ya uhuru na kuzifanyia kazi changamoto kwa kuzitolea ufumbuzi wake ili taifa letu liendelee mbele zaidi na kuwa taifa lenye maendeleo ya uchumi wa kati.
Kwa wanachi wenzangu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tuweke nia na ari katika kujenga uchumi wa taifa letu kwa kufanaya kazi kwa bidii na kutekeleza wajibu wetunkila mmoja katika upande wake tutapata taifa la wachapakazi na wapenda maendeleo. Tuamke tuwe imara twende na kasi ya maendeleo ya dunia kwa sasa. Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John pombe Joseph Magufuli kwa kauli mbiu yake anasema “HAPA KAZI TU”  basi tufanye kazi kwa maendeleo yetu na taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.