Tanzania yaanza rasmi sheria ya makosa ya mtandao


Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bunge la jamhuri ya Muungano wa TanzaniaSerikali ya Tanzania ilitoa tamko maalum la kuanza utekelezaji rasmi wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015  na sheria ya miamala ya kielektroniki ambayo imekuwa gumzo kubwa  tokea kupitishwa sheria hizo huku wengi wakiiona kwamba itanyima uhuru wa kutoa na kupata habari

Tamko la kuanza utekelezaji rasmi wa sheria hizo mbili yaani ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015  na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015  lilitolewa na Wizara ya Mawasilaiano, Sayansi na Teknolojia kupitia waziri wake, Profesa Makame Mbarawa. Sheria hizo zinaanza kutumika rasmi kuanzia Jumanne yaani Septemba mosi mwaka huu.
Profesa Mbarawa alisema licha ya kuwepo mafanikio katika  matumizi ya mitandao, changamoto zilizojitokeza zilifanya serikali kutunga sheria hizo mbili. 
​Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam,  Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema hakuna ukweli wowote kwamba sheria hizi mbili zimeletwa ili kudhibiti uhuru wa mawasiliano kwa watanzania hususan wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu ujao  na kwamba wamejipanga ili kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda kwa haki.
Kuanza kwa utekelezaji wa sheria hizi mbili za  makosa ya mtandao ya mwaka 2015  na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015 kunatokana  na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha hatua hiyo hapo April mosi mwaka huu.