SI NIMEOTA NIMEKATWA


Kitime-191x300Dah ndoto jamani ndoto kitu cha ajabu sana. Ndoto hizihizi watu wengine ndio huwa wanatumia kama dira ya maisha, wakiota ndoto tu basi mapema kesho yake wanakuwa na kazi ya kutafuta maana ya ndoto. Dunia nzima kumejaa wataalam mabingwa wa kutafsiri ndoto. Ukiota unapaa, mtaalamu mmoja atakwambia hiyo ni dalili kuwa matatizo yako yote yamekwisha, mwingine atakwambia kama umeota unapaa ujue basi unalogwa, mwingine atakwambia hiyo maana yake maadui zako hawakupati tena, basi kasheshe tupu.
Kuna maelezo mengine kuwa ndoto ni matokeo ya kumbukumbu mbalimbali za mambo yaliyotutokea au kusikia au kuyaona au hata kuyahisi, kwa hiyo ndoto hazina tafsiri ni ubongo tu unafanya kazi ukiwa umelala. Lakini jamani hii ndoto niliyopata wiki hii lazima ina maana yake. Baada ya kutoka katika mihangaiko yangu nikaingia kitandani kulala, katikati ya usingizi si nikaanza kuota, nikajikuta nashuka kwenye gari la bei mbaya lenye full kiyoyozi. Moja kwa moja nikaingia katika ukumbi uliojaa watu ambao nikawa najua ni Halmashauri Kuu ya Kamati Kuu ya chama changu cha siasa. Na mkutano ule ulikuwa wa kumpitisha mtangaza nia ili awe mgombea urais, na mimi nilikuwa mmoja wa watangaza nia. Ile kuingia tu watu wote wakasimama na kuanza kunishangilia kwa nguvu na kunipigia makofi. Nikawapungia mikono tena hapo nikaanza kutembea slow moshen kama kwenye kwenye sinema, nikiwapungia mkono wajumbe wa mkutano huo. Baada ya kukaribishwa kwenye kiti changu na mabinti waliopendeza kwa yunifom za chama changu. Nikawekewa mbele yangu soda na mazagazaga mengine na kukaribishwa kuanza kula, ukumbi mzima walikuwa wakitaja jina langu na misifa kibao, mkombozi, shujaa, kiboko yao, Mzee Chekanakitime wa ukweli. Kiukweli ilikuwa wazi mimi ndie chaguo la watu, nakumbuka nikaanza kupanga watu wa kuwakaribisha siku ya kuapishwa, na pia nikaanza kupanga listi ya watu wa kuwashughulikia nikishaapishwa tu. Si unajua watu wengine vimeo. Niwe mkweli nilianza kupanga michepuko gani ntaanza nayo wiki ya kwanza ya utawala wangu.
Mwenyekiti wa chama changu akaniomba niongee na wajumbe ambao ni wazi walikuwa wamejawa na mapenzi makuu na imani juu ya uongozi wangu, niliwaahidi nitawakumbuka mara baada ya kuapishwa. Nilidhamiria nikipewa rungu tu, nabadili katiba ili wajumbe hawa wawe wa kudumu maana walionyesha uzalendo mkubwa kwangu na kwa chama chetu kitukufu. Kuna binti mmoja alikuwa na shepu nzuri sana na alikuwa anacheza na kuimba kwa furaha , huyu nilijiwekea nadhiri nitampa ukuu wa mkoa au Ubunge wa kuteuliwa, mpiga debe wangu msanii maarufu nitampa kawilaya. Kuna kagazeti fulani kanajifanya kananifuatilia sana maisha yangu, wiki ya kwanza tu nakafungia, na kale kachoraji kavikatuni kwenye gazeti lile ntakatia ndani kakajifunze kazi ya uashi kule gerezani.
Nilikatishwa mawazo kwa kushtuliwa na kuambia kuwa ni muda wa wajumbe kupitisha majina ya wagombea rasmi, hivyo mimi na watangaza nia wengine wengine tutoke nje na kusubiri matokeo. Wakati tunatoka nikawa nasikia wajumbe wakipiga makofi na kulitaja jina langu, niliwaonea huruma watangaza nia wenzangu maana nilijua wananisindikiza tu. Muda si mrefu tukaitwa ndani nikawa tayari kusherehekea kwa nguvu, Mwenyekiti wetu kaongea machache akaanza kutaja waliokatwa si akanitaja na mimi, nikashtuka mpaka usingizi ukapea, nikajikuta niko ghetto kwangu. Ndoto hii maana yake nini wataalamu?

Related Posts