RC GAMA AKANA KUFANYA UDALALI WA ARDHI



 Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ,Leonidas Gama akizungumza na wanahabari (hawako pichani) juu ya tuhuma zilizoibuliwa bungeni dhidi yake.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama akiwa na mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga katika mkutano huo na wanahabari.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali ya habari mkoani Kilimanjaro.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

SIKU moja baada ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kumlipua mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama kwa madai ya kufanya udalali na ufisadi katika uporaji wa ardhi ya wananchi ,mkuu huyo amejitokeza
mbele ya wanahabari na kukanusha tuhuma hizo.

Katika utetezi wake Gama alirejea kauli yake aliyoitoa miaka sita iliyopita ya kuwa yeye ni msafi huku akiitupia mzigo halmashauri ya wilaya ya Rombo tuhuma za kiasi cha sh Mil 500 zilizotajwa kutolewa wawekezaji wa Kichina kama fidia kwa wananchi katika ardhi
kilipojengwa kiwanda cha kutengeneza Saruji.

Alisema tuhuma zilizotolewa Bungeni dhidi yake si za kweli na kwamba ni za kisiasa huku akitaja sababu ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni kutokana na juhudi zake za kupambana na Pombe haramu katika wilaya ya Rombo pamoja na Urejeshwaji wa wafanyabiashara katika soko la kati la mjini Moshi.

“Nataka niwaambie hii ni siasa,zipo issue nyingi zilizochangia kuibuka kwa haya mambo ,lakini nawaambieni mbili tu,Issue ya kwanza Pombe Rombo,na msimamo wangu juu ya Pombe Rombo ndio imeza hii,la pili ni
soko la Moshi mjini,watu wana agenda zao kwenye soko hilo ,wananchi wamerudi pale ,imewaumiza watu.”alisema Gama.

“Watu walitaka Pombe ya Gongo iharalishwe,mimi nimesema hadharani anayetaka pombe ya Gongo ihararishwe si mwenzetu mu mshughulikie kwa maana si mwenzetu sasa hili limeleta nongwa”aliongeza Gama.

Akitoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo ,Gama amekiri mtoto wake aliyetajwa kwa jina la Mayunga Leonidas Gama kuhusika katika uanzishaji wa kiwanda hicho huku akihakikisha kiwanda hicho kinajengwa katika mkoa wa Kilimanjaro badala ya Bagamoyo kama walivyo pendelea
wawekezaji hao.

“Kiwanda cha saruji kinachojengwa pale Rombo, nilikuwa na uwezo wa kukipeleka popote ninapotaka mimi, lakini mimi binafsi ndiye niliyefanya juhudi kiwanda kile kijengwe Kilimanjaro, mimi binafsi na wala sio mtu mwengine, nimefanya juhudi hizo kwa lengo la kuongeza
ajira kwa wananchi na kuinua uchumi wa mkoa huu”, alisema Gama .

“Historia ya Kiwanda hiki iko wazi, na  nililipeleka hadi kwenye kikao cha ushauri wa mkoa (RCC),nanaomba nieleweke kwamba, ni juhudi zangu na za mtoto wangu, nilitamka kwenye kikao kile na wala sikuficha, mtoto wangu ambaye ametajwa yeye ana rafiki yake wa kichina, wala si
kweli kwamba hii kampuni mimi nimekwenda kuichukua China kwa gharama za serikali” aliongeza Gama.

Alisema katika kikao hicho (RCC), Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Vunjo, Dkt. Augustino Mrema na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, walishiriki katika kikao hicho na kwamba baada ya mvutano ndipo makubaliano yakawa kiwanda kijengwe wilaya ya Rombo .

“Toka siku ile mimi kama mkuu wa mkoa nikakabidhi madaraka wilaya yaRombo,kwa hiyo shughuli zote za ujenzi ,shughli zote za kutafuta viwanja ziifanywa na halmashauri ya wilaya ya Rombo na sio Gama”alisema Gama.

Alisema waliolipa fidia na kununua viwanja ni halmashauri ya wilaya na hata eneo kilipojengwa kiwanda hicho ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Rombo na si cha mwekezaji kama inavyoelezwa .

“Nimeelezwa kweye tuhuma kuwa nimepewa milioni 500,hii ni hadithi ya kisiasa ,sijapokea kiasi hicho cha fedha wala sikijui,hata hizo hisa 20,000 nilizoambiwa ninazo kwa kweli sina ,kama ningekuwa nazo ni haki yangu kwa sabau sijavunja sharia lakini sin ahata hisa moja.”alisema
Gama.

“Swala mtoto wangu kuwa na hisa si dhambi na ni haki yake kisheria,kwa
sababu yeye ndiye aliyewatafuta hao watu na ni rafiki zake ,wala si
mimi niliyewaleta kama amenunua hisa huko ni hiari yake,mimi sina hisa
kama Gama,sijapokea milioni 500 kama gama,mimi si dalali na kama ni
udalali wa ardhi hiyo itakuwa ni halmashauri ya wilaya ya Rombo na si
gama.”alisema Gama.

Alipoulizwa endapo kama halmashauri ya wilaya ya Rombo itakuwa inamiliki sehemu ya hisa katika kampuni hiyo kutokana na utolewaji wa ardhi yake ,Gama alisema wenye majibu ni halmashauri ndio watakuwa wanajua ni mikataba gani wameingia na wawekezaji hao.

Kuhusu eneo la Uwekezaji wa soko la Lokolova, Gama alisema ameshangazwa na kauli za kuwa yeye ni fisadi wa ardhi katika eneo hilo wakati makubaliano ya kuanzishwa kwa soko la kimataifa na ji mdogo wa kibiashara ulipitishwa katika kikao cha RCC ambacho pia Mbunge wa Vunjo, Dkt. Augustino Mrema alihudhuria na kusifia mpango huo.

Sakata la Kiwanja cha Mawenzi, Gama alisema yeye kama mkuu wa Mkoa, alichokifaya ni kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kufuata Sheria za umilikishwaji wa Ardhi ili kuepusha Halmashauri kufilisiwa kwa kukiuka taratibu.

Juzi wakati akiwasilisha bungeni maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu bajeti yay a wizara ya ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi kwa mwaka wa fedha 2015/2016,msemaji mkuu wa kambi hiyo Halima Mdee
alimrushia tuhuma Gama za kuhusika katika kutumia fedha za serikali kwenda nchini China kutafuta watu wawili wanaotajwa kama wawekezaji.

Katika taarifa hiyo Mdee alidai katika hali isiyo ya kawaida nay a kushangaza watu hao katika ardhi iliyokwisa lipiwa fidia kwa fedha za umma ,ilianzishwa kampuni binafsi ya Jun Tu Investment International Company Ltd .