Maajabu Mto Kiwira, ‘The Natural Bridge!”


After watching “Enter the Dragon” by Bruce Lee, it is time now you go for the real dragon, as believed by locals, at Kiwira Natural Bridge in Rungwe District, Mbeya Region, about 900km from Dar es Salaam City to the site in the Southern Highlands of Tanzania!
  • Kutoka Atanyelite Bukomu hadi Daraja la Mungu
  • Ni mto wenye vivutio lukuki, vikiendelezwa watalii wataongezeka maradufu
 KAMA umewahi kuangalia filamu iliyompandisha chati marehemu Bruce Lee, “Enter the Dragon,” basi tembelea Mto Kiwira ukakutane na dragon wa kweli, si yule wa kwenye filamu. Ila utahitaji moyo, kwani wengi hupotelea huko, hivyo hakuna anayerudi kusimulia alivyokutana naye
Lakini yote hayo, mwanzo wake ni wezi wa mifugo, wao walifurahia kugundua kivuko kwa ajili ya kuvusha mifugo yao waliyoiba kwenye Bonde la Usangu, pasipo kufahamu, walikuwa wameibua neema kwa vizazi vyao vya leo katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Kivuko hicho si kingine, ni Daraja la Mungu, (God’s bridge au natural bridge) likiwa limegunduliwa na wezi hao zaidi ya miaka 100 iliyopita kilipo Chuo cha Magereza Kiwira, katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Daraja hili ni moja ya vivutio kadhaa vya utalii vilivyomo kwenye Mto Kiwira. Vivutio hivyo ni miongoni mwa maajabu kwenye mto huo, na wenyeji wanayahusisha na uwezo wa Mwenyezi Mungu unaojidhihirisha katika umbaji.
Pamoja na Daraja la Mungu kipo kivutio cha kijungu na maporomoko. Na kipo kivutio kingine katika simulizi za wenyeji ambacho kinaelezwa kuwa chanzo cha wezi wale wa mifugo kuligundua daraja hilo.
Wezi walivyogundua daraja;
Simulizi za wenyeji kuhusu daraja hilo ni kivutio tosha kwa mtalii au msikilizaji awaye yeyote. Katika simulizi hizo inaelezwa na wenyeji kuwa, walitoka kwenda kuiba mifugo katika Bonde la Usangu, wenyewe wanalitambulisha zaidi kama kwa “Chifu Merele.”
Miongoni mwa mifugo waliyoiba huko ni ng’ombe pamoja na mbuzi. Na wenye mifugo walipowafuatilia walikabiliwa na kikwazo cha kuvuka Mto Kiwira unaotenganisha upande wa Mashariki liliko Bonde la Usangu na vijiji vyao vilivyokuwa Magharibi ya mto huo.
Nilifanikiwa kukutana na Paison Ndonelo Katika Kijiji cha Kijungu. Yeyey ni Afisa Maliasili Misitu, Wilaya ya Mbarali na mzaliwa wa Kijungu. Ana masimulizi ya kutoka kwa wazazi wake kuhusu kugundulika kwa daraja hilo zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Ndonelo anasema, kwa mujibu wa fasihi simulizi ya wazee wa kijiji hicho, ni kwamba wenyeji wake ambao ni wa jamii ya Wandali na Wanyika walikuwa na kawaida ya kwenda kwenye Bonde la Usangu, ambako kulifahamika zaidi kwa jina la mtawala wake, Chifu Merele.
Katika safari hizo waliiba ng’ombe wa wenyeji wa Bonde hilo na kusafiri nao hadi kijijini kwao, na ili kuingia kijijini, Magharibi ya mto, walilazimika kuvuka Mto Kiwira. Walitumia eneo ambako kingo za mto huo zilikaribiana, wakiamini ziko karibu sana kiasi cha wao kuruka tu.
Hata hivyo, Wasangu nao waliweza kufuatilia mifugo yao iliyoibwa, na walipofanikiwa kuwakuta wezi wao wakiwa hawajavuka, wezi nao hawakuwa tayari kuachia vyote, yaani ng’ombe na mbuzi.
“Walijifunga kamba kiunoni na mbuzi kasha kuruka nao kwenye eneo waliloamini ni finyu hivyo wangeweza kuruka. Lakini hakuna aliyefanikiwa. Walitumbukia mtoni. Hawakushituka.
Waliendelea huku kila mmoja akimuona mwenzake kuwa hakuruka vizuri,” anasimulia Ndonelo.
Kisa hicho kinaelezwa kuwa chanzo cha utani miongoni mwa Wandali mkoani Mbeya, wakisema;
“Atanyelite bukomu,” ikiwa na maana kwamba hakuruka vizuri, lakini pamoja na kuwepo utani huo bado simulizi hii ya wizi wa ng’ombe, haizungumzwi.
Simulizi hii inaelezea kuwa kila aliyejaribu kuruka ili avuke eneo hilo waliloamini kuwa lilikuwa si pana, alitumbukia mtoni. Wenyeji waliamini kwamba watu waliokuwa wakijaribu kuruka walitumbukia na kupotea kwa sababu kingo za mto zilitanuka pale mtu aliporuka.
Hatimaye wananchi hao walibaini kuwa haiwezekani kuvuka eneo lile kwa kuruka, na ndipo walipoanza kutafuta eneo jingine la kuvukia, wao na mifugo waliyoiba Usangu.
“Walianza kuteremka chini kutafuta. Enzi zile eneo hili lilifunikwa. Kulikuwa na pori kubwa, walianza kutafuta kuelekea chini ya mto yanakoelekea maji. Wakagundua huo mwanya, wakaendelea kupapasa, na kuangalia wakashangaa wanavuka ng’ambo na ndipo ukawa mwanzo wa kugundulika kwa Daraja la Mungu,” anasimulia Ndonelo.
Ugunduzi wadaraja hilo ulikuwa muujiza kwa wananchi hao, na ndiyo sababu ya kuliita Daraja la Mungu, au ‘ululalo lwa Kyala,’ kama linavyofahamika kwa Kindali.
Eneo hilo sasa limejengwa daraja linaounganisha Chuo cha Magereza na upande wa pili wa kijiji hicho.
Imani za wenyeji juu ya Mto Kiwira;
Pamoja na simulizi hiyo ihusuyo daraja hilo, wenyeji wanaamini pia kuwapo kwa joka kubwa (dragon), ambaye kwa lugha yao huitwa NYIFWILA.
Lakini kuna maelezo tofauti kuhusu vichwa vyake. Baadhi hudai kuwa na vichwa 12 na wengine, hususan wazee, hudai kuwa joka hilo lina vichwa saba.
“Nyoka yupo kwenye daraja la Mungu, ana vichwa saba, anavitawanya, hata hapa Kijungu yupo lakini mdogo, ni moja ya vichwa cha yule mkubwa,” anasema mzee Eliah Kabagafya.
Mzee Kabagafya (88), anasema si rahisi kuliona joka hilo, bali muda wa jioni huwapo mwanga mkali unaoaminika kuwa unatokana na joka hilo.
Kwa mujibu wa wenyeji hao, joka hilo huweza tu kuonekana kwa kutumia vifaa maalumu vya kisasa au kwa nguvu za wazee wa kimila.
Wenyeji wanaamini kuwa hatma ya Wilaya ya Rungwe iko katika uhai wa joka hilo hapo Daraja la Mungu, kama anavyosimulia Mzee Kabagafya, kwa Kinyakyusa akisema:
“Lengha jisokilepo ikisu kikusenuka.” Ambayo maana yake kwa Kiswahili inakaribiana na:
“Iwapo joka hilo litaondoka hapo Daraja la Mungu basi eneo hilo litadidimia au kuangamia.”
Kutokana na imani kuhusu maajabu ya daraja hilo, wenyeji waliwaleta watuhumiwa wa uchawi eneo hilo wakiamini kuwa mtu yeyote aliyeshiriki vitendo vya kichawi asingeweza kuvuka kwenye daraja hilo, walitumbukia mtoni na kuangamia.
Taarifa zisizo rasmi kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo zinabainisha
angalau kila mwaka kuwepo kwa mtu anayetumbukia darajani hapo na kupotelea mtoni kwa kusombwa na maji.
Kumbukumbu iliyopo ni ya raia mwenye asili ya India ambaye inaelezwa alitumbukia darajani hapo na kupotelea Mto Kiwira pamoja na mtoto wake, Februari 08, mwaka 1972. Kwa kumbukumbu ya tukio hilo,imewekwa alama ya jiwe ikionyesha tarehe lilipotokea.
Afisa Utalii Wilaya ya Rungwe, Numwagile Bugali anasema raia huyo mwenye asili ya India alifika eneo hilo akiwa na familia yake, mke na mtoto. Katika miaka hiyo ya 70 palikuwa na eneo la mapumziko, “Natural Bridge Campsite,” na katika tukio hilo inaelezwa kuwa ni mama pekee aliyepotea.
daraja la Mungu2 Alama ya jiwe, kama inavyonekana pichani, imewekwa kwenye daraja hilo ikielezwa kuwa kumbumbu ya kupotea kwa raia huyo mwenye asili ya India eneo hilo baada ya kusombwa na mkondo wa maji.
“Yule mhindi nyakati za jioni alishuka, yeye, mke na mtoto wake kwenda kuogelea japo kuwa alionywa na wenyeji kuwa hilo eneo ni hatari.
“ Walivyokuwa wakiogelea mtoto alichukuliwa na maji, baba akajaribu kumuokoa mtoto, naye akapotelea majini, ni mke pekee alipona,” anasema Numwagile.
Daraja la Mungu liliumbika takribani miaka milioni 1,800 iliyopita ikiwa ni matokeo ya uji au tope la volcano ambalo lilichanganyika na maji na hatimaye kuumbika kwa umbo hilo la jiwe kwenye Mto Kiwira ambalo leo hii linatambulika kama Daraja la Mungu.
Kivutio hiki ni moja ya vyanzo vya mapato kwa Kijiji cha Kijungu ambapo kila mtalii anayetembelea hapo hutozwa shilingi 5,000.
Daraja hilo linatenganishwa na kivutio kingine kilichopo eneo hilo kwenye Mto Kiwira kwa kilometa nane, nacho ni kivutuo kinachofahamika kwa jina KIJUNGU.
daraja la Mungu 1 Pamoja na daraja hilo la asili, kivutio kingine kilichopo eneo hilo ni maporomoko ambayo pamoja na majabali yaliyopo na msitu hutengeza mandhari ya kipekee yenye kuvutia kama inavonekana pichani.