Burundi;Watoto Wakimbizi wanadhulumiwa


Burundi;Watoto Wakimbizi wanadhulumiwa
Shirika la kutoa misaada la Save the Children limesema kuwa zaidi ya watoto elfu mbili mia tatu 2,300 ambao hawana wazazi, wamekimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi.
Shirika hilo limesema kuwa baadhi ya watoto hao walitembea kwa miguu kwa muda wa wiki moja hadi mataifa jirani ya Rwanda, Tanzania na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msemaji wa shirika hilo la Save the Children, Edwin Kuria,amesema idadi kubwa ya watoto hao walifika katika kambi za wakimbizi wakiwa hawana hata viatu na mali waliyokuwa nao ni mavazi tu waliokuwa nayo mwilini.
Uhasama wa kisiasa unaoendelea Burundi umesababisha taharuki miongoni mwa wenyeji
Tangu aprili mwaka huu watoto wengi kutoka Burundi wamekuwa wakitembea hadi kambi hizo za muda nchini Rwanda,Tanzania Uganda na DRC.
Shirika hilo limeonya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka huku wengi wakitoroka Burundi wakihofia kuzuka kwa mapigano.
Taifa hilo linajianda kwa uchaguzi mkuu ambao awali ulipangiwa kuandaliwa mwezi huu.
Aidha shirika hilo limesema watoto hao wanakabiliwa na matatizo mengi njiani na wanapofika katika kambi hizo ambazo kwa sasa zimefurika usalama wao bado sio shwari.
Baadhi ya watoto hao wameripotiwa kunyanyaswa na kudhulumiwa na wakaazi wa maeneo hayo.
Watoto wameathirika sana na kipindupindu
Watoto hao hawaendi shuleni na sasa jukumu lao kuu ni kukusanya kuni au kuchimba vyoo majukumu ambayo sio salama kwa watoto amesema bwana Kuria.
Katika kambi ya Mahama nchini Rwanda watoto hao wanakabiliwa na matatizo ya kupata maakazi ya kuishi na pia maji safi ya kutumia.
Nchini Tanzania katika kambi ya Nyarugusa, idadi ya watoto wanaogonjeka imeongezeka hasa kufuatia kufungwa kwa vituo viwili ya muda kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.