LICHA ya serikali kupiga marufuku shule yoyote kuwafukuza wanafunzi wake kwa sababu ya kutolipa ada, zaidi ya wanafunzi 60 wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Seminari ya kidugala, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT), wamefukuzwa kwa madai ya kutolipa ada na michango.
Miongoni mwa michango ambayo wanafunzi hao wanadaiwa ni pamoja na mchango wa kununulia basi, mchango wa kambi wakati wa likizo ya mwezi wa sita, na mingine.
Uhuru imeshuhudia wanafunzi wakihangaika kuwasiliana na wazazi wao, baada ya kushushwa Njombe mjini toka katika kijiji cha Kidugala, iliko shule hiyo ili watumiwe nauli.
“Tunahangaika kuwatafuta wazazi wetu walio mbali na Njombe ili watutumie nauli turudi nyumbani kwa sababu tumelipa ada kidogo, sio milioni 1.7 wanayoitaka walimu,mimi nimelipa Sh laki nane lakini nimefukuzwa,”alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Walisema michango yete ni zaidi ya Sh 560,000 huku ada ikiwa sh milioni 1.5 kiasi ambacho wazazi vijijini hawawezi kulipa yote kwa mara moja, kama walimu wanavyotaka.
Wanafunzi hao walisema lengo la seminari hiyo kujengwa ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi wa familia duni, kupata elimu ya sekondari na sio kufanya biashara.
Wazazi wa wanafunzi hao waliiomba serikali kuingilia kati tatizo la walimu wa shule hiyo kuwafukuza wanafunzi, na kuwatelekeza mijini jambo ambalo ni hatari.
“Unapomfukuza mtoto bila kuwasiliana na mzazi unataka afanye nini, tunasikitishwa na jambo hili,” alisema Anitha Mgeni, mkazi wa mtaa wa Mgendela, Njombe mjini baada ya kuwapokea watoto watatu, akiwahifadhi nyumbani kwake ili wawasiliane na wazazi wao.
Mzazi huyo alidai kuwa shule hiyo ilijengwa na waumini wa KKKT kwa lengo la kuwasaidia watoto wa watu maskini, lakini kwa sasa imekuwa ikitoza ada kubwa kuliko matarajio ya waumini hao.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Kidugala, Jackson Ngilangwa alikiri wanafunzi wengi kudaiwa ada, na kwamba hakuwepo shuleni wakati wanafunzi hao wanafukuzwa.
Akizungumza kwa njia ya simu, Ngilangwa alisema michango na ada ambazo wanafunzi hao wanatakiwa kulipa ni ile ya msingi.
“Mimi nipo kwenye semina sipo shuleni, ngoja niwasiliane na makamu mkuu wa shule kuona kwa nini amewafukuza wanafunzi hao,”alisema.